Katika kile kinachoonekana kuchoshwa na vitendo vya polisi kuwaua watu weusi huko nchini Marekani, Raia wa nchi hiyo wamefanya maandamano makubwa kupinga kadhia hiyo wanayofanyiwa watu weusi wasio na hatia. Katika maandamano hayo, baadhi ya waandamaji wakiwa na walenga shabaha (sniper) waliwaua polisi watano.
Tukio hilo limetokea jijini Dalas, jimboni Texas ambapo polisi hao watano waliuawa na wengine sita kujeruhiwa. Mapambano kati ya polisi na raia hao bado yanaendelea na taarifa zinasema kuwa kuna mshukiwa mmoja wa walenga shabaha amejibanza katika eneo la kuegesha magari ndani ya jengo moja na amewasiliana na maafisa wa polisi akiwaeleza kuwa wasipoangalia atawaumiza na kuwaua wote kwani ametega mabomu kuzunguka eneo hilo.
Mkuu wa polisi wa Dallas, David Brown, amesema wanawashikilia watuhumiwa ingawa si wote. Vyombo vya habari vya jimbo hilo vinasema kumetokea mlipuko mkubwa eneo hilo, lakini habari hizo hazijathibitishwa. Mkuu huyo wa polisi anasema wanamuhoji mwanamke mmoja ambaye alikuwa eneo ambalo mshukiwa ambaye bado anarushiana risasi na polisi amejibanza.

Maandamano haya yamekuja baada ya kuuawa kwa wanaume wawili weusi, Philando Castile wa jimbo la Minnesota na Alton Sterling wa eneo la Baton Rouge jimboni Louisiana.
Raisi wa Marekani, Barack Obama, akirejea takwimu zinazoonesha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa Wamarekani weusi kupigwa risasi na maafisa wa polisi kuliko Wamarekani wazungu, amesema kuwa ubaguzi huo unafaa kumalizwa.
''Visa kama hivi vinapotokea kuna sehemu kubwa ya raia wanaohisi kwamba hawatendewi haki kwa sababu ya rangi ya ngozi zao, kwa sababu hawatizamwi kwa njia sawa, na hili linauma''alisema.
No comments:
Post a Comment