Na Samwel Mtuwa, GST
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) imetoa taarifa kwa wananchi kuhusu
tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 13 Julai, 2016, majira ya saa 12:01:15
alfajiri , likiwa na ukubwa wa kipimo cha Ritcher 5.1.
Kitovu cha tetemeko hilo kilitokea umbali wa kilomita 11 Mashariki mwa mji
wa Haneti ambao upo umbali wa kilomita 79 Kaskazini Mashariki mwa mji
wa Dodoma.
Akizungumza na MEM Bulletin ofisini kwake, Mtalaam wa Matetemeko
katika Idara ya Jiolojia, GST, Gabriel Mbogoni, alisema kuwa eneo hilo lipo
katika ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, maeneo hayo
hukumbwa na matukio ya matetemeko ya ardhi mara kwa mara.
Akifafanua kuhusu chanzo cha tetemeko, Mbogoni alisema kuwa hiyo ni
kutokana na tabaka la miamba katika maeneo hayo kuwa na kina kidogo
ikilinganishwa na maeneo ambayo yako nje ya ukanda wa Bonde la Ufa.
“Hali hii husababisha matabaka ya miamba katika ukanda huo kuwa katika
hali ya fukuto jingi la joto na kusigana kwa miamba ambapo husababisha
miamba hiyo kukatika, hali ambayo hufanya ardhi itikisike,” alisema
Mbogoni.
Alisema kuwa kiutalaam hali hiyo husababisha miamba hiyo kukatika na
kusababisha mtikisiko wa ardhi ambao ndio huitwa tetemeko la ardhi.
Akieleza kuhusu madhara ya tetemeko hilo, Mbogoni alisema kuwa mpaka
muda wa mchana wa siku ambayo tetemeko lilitokea, hakukuwa na taarifa
yoyote ya madhara kwa wananchi, majengo au miundombinu iliyotolewa
kutokana na tetemeko hilo.
Alifafanua kuwa eneo la Haneti kijiografia lipo katika ukanda wa Bonde la
Ufa, maeneo ambayo yana mipasuko mingi ya miamba.
Alisema kiutalaam mawimbi ya tetemeko la ardhi yana tabia ya kusafiri
umbali mrefu katika mwendo wa kasi alitolea mfano mawimbi ya P na S
yanaweza kusafiri umbali wa kilomita 8-13 kwa sekunde.
Akizungumzia kuhusu tahadhari, Mbogoni alisema kuwa, wananchi
wanaposikia hali ya kutokea kwa Tetemeko la Ardhi wanapaswa kuchukua
tahadhari ya kukaa mbali na miti, nguzo za umeme na nyumba ndefu kama
vile maghorofa, na pindi wanapokuwa ndani ya nyumba wanashauriwa
kukaa katika kona za ukuta wa nyumba ili kujizuia na madhara.
Moja ya majukumu ya GST ni kufanya uchunguzi juu ya matetemeko,
maporomoko, mipasuko ya ardhi katika eneo zima la nchi, kwa sasa GST
ina vituo tisa ya kurekodi taarifa zote za matetemeko katika mikoa
mbalimbali ya nchi kama vile Dodoma, Arusha, Babati, Singida, Geita,
Kibaya, Kondoa , Mbeya na Mtwara.
No comments:
Post a Comment