HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 3, 2016

TOZO DARAJA LA NYERERE YAJADILIWA

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Joseph Nyamhanga amewataka watumiaji wa Daraja la Nyerere (Kigamboni) kuzingatia matumizi bora na sahihi ya daraja hilo ikiwemo usafi ili kuliwezesha kukidhi matarajio ya serikali na kudumu kwa muda mrefu.

Akizungumza katika kikao maalum cha wadau kutathimini viwango vya tozo vitakavyotumiwa katika daraja hilo Eng. Nyamhanga amewataka waendeshaji wa daraja hilo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuimarisha huduma ya ulinzi na usalama na kuwataka watumiaji wa daraja hilo kutumia fursa za uwepo wake kiuchumi na kijamii.

“Hakikisheni tozo zitakazowekwa ziwiane na hali ya maisha ya wananchi ili kuwavutia wengi kupita katika daraja hili na kupunguza msongamano katika vivuko”, amesema Eng. Nyamhanga.Tozo hizo ambazo zitaanza kutozwa kwa watumiaji wa Daraja la Nyerere hivi karibuni zinalenga kuwezesha NSSF kurudisha gharama za uwekezaji katika daraja hilo.

Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhujumu miundombinu na kukemea vitendo vya watu kufanya biashara katika daraja hilo.Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Profesa Godius Kahyarara amesema tozo kwa watumiaji wa Daraja la Nyerere itaanza hivi karibuni baada ya kupitishwa na Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, hivyo amewataka watumiaji wa daraja hilo kutoa ushirikiano kwa watendaji ili kuwezesha huduma kufanyika kama ilivyokusudiwa.

“Tumejipanga Vizuri na tutaanza kutoza watumiaji wa Daraja la Nyerere muda mfupi kuanzia sasa.” amesema Prof. Kahyarara.Zaidi ya shilingi Bilioni 214 zimetumika katika ujenzi wa Daraja la Nyerere ambapo asilimia 60 zimegharamiwa na NSSF na asilimia 40 zimegharamiwa na Serikali Kuu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga (katikati) akitoa ufafanuzi kwa wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji katika kikao cha kujadili viwango vya tozo zitakazotumika katika Daraja la Nyerere (Kigamboni). Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof Godius Kahyarara na kushoto ni Mkurugenzi wa barabara (Ujenzi) Eng. Ven Ndyamukama.
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Baiskeli akitoa maoni ya namna ya kuwahudumia waendesha baiskeli katika kikao cha kujadili tozo zitakazotumika kataka Daraja la Nyerere.

Wadau wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kujadili tozo zitakazotumika katika Daraja la Nyerere, Tozo hizo zitatangazwa hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad