Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akisaini leseni ya madini itakayoiwezesha kampuni ya Edenville International (T) Ltd kuchimba makaa ya mawe katika eneo la Mkomolo na Namwele mkoani Rukwa kwa ajili ya kuzalisha umeme. Wanaoshuhudia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (wa pili kulia), Kamishna Msadizi wa Madini anayeshughulikia Wachimbaji Wadogo, Julius Sarota (wa kwanza kulia), Mwanasheria wa Wizara, Abbas Kisuju (kushoto kwa Waziri) na Mhandisi Joseph Kumburu (kushoto kwa Mwanasheria).
Watendaji kutoka kampuni ya Edenville (T) Ltd wakishuhudia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa kwanza kulia), akisaini leseni ya madini itakayoiwezesha kampuni hiyo kuchimba makaa ya mawe katika eneo la Mkomolo na Namwele mkoani Rukwa kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 300. Kutoka kushoto mstari wa mbele ni Gwakisa Mwakyusa, Cassiano Kaegele, Mohj Pryor na Peet Meyer.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akisisitiza jambo mbele ya Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Taasisi na kampuni ya Edenville (T) Ltd kabla hajasaini leseni inayoiruhusu kampuni hiyo kuchimba makaa ya mawe katika eneo la Mkomolo na Namwele mkoani Rukwa kwa ajili ya kuzalisha umeme wa megawati 300. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Sekta ya Madini, Profesa James Mdoe (hayupo pichani) na Kamishna Msadizi wa Madini anayeshughulikia Wachimbaji Wadogo, Julius Sarota (hayupo pichani).
Na Teresia Mhagama.
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesaini leseni ya madini itakayoiwezesha kampuni ya Edenville International (T) Ltd ambayo ni kampuni tanzu ya kampuni ya Edenville Energy PLC ya nchini Uingereza kuchimba makaa ya mawe katika eneo la Mkomolo na Namwele mkoani Rukwa kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Utiaji saini wa leseni hiyo ulifanyika jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Wizara ya Nishati na Madini na kushuhudiwa na watendaji mbalimbali wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Sekta ya Madini, Profesa James Mdoe pamoja na watendaji wa kampuni ya Edenville.
Naibu Katibu Mkuu, Profesa James Mdoe, alisema kuwa baada ya kupatikana kwa leseni husika kampuni hiyo itaanza kazi ya kuchimba madini hayo ya makaa ya mawe ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
“Baada ya kuanza kuchimba makaa hayo mwezi Juni, kampuni hii imelenga kujenga mtambo wa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 300 katika kipindi cha kati ya miezi 20 hadi 22 baada ya kupata cheti cha mazingira kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira,” alisema Profesa Mdoe.
Alisema kuwa umeme huo wa megawati 300 utazalishwa katika kipindi cha miaka 35 kwa kutumia hifadhi ya makaa ya mawe ambayo Kampuni hiyo imethibitisha kuwepo katika leseni yao kwenye eneo la Mkomolo, mkoani Rukwa ambayo yanafikia tani milioni 173.
Alieleza kuwa kiasi hicho cha umeme kinaweza kuongezeka endapo watagundua mashapo zaidi ya makaa ya mawe katika eneo lao lingine la Muze ambalo linaonesha dalili ya kuwa na makaa ya mawe mengi na lipo karibu na eneo la Mkomolo.
Naibu katibu Mkuu alisema kuwa katika kikao hicho wamekubaliana na kampuni ya Edenville kutekeleza masharti yote yaliyopo ndani ya leseni ikiwemo kutekeleza kazi zote zilizopangwa kufanyika kama Mpango Kazi wa kampuni hiyo unavyoelekeza.
“Tumewahimiza waishi maneno yao, mfano hapa wameeleza kuwa wanatarajia kuanza kuchimba makaa ya mawe mwezi Juni mwaka huu, inabidi watekeleze suala hilo ili mwisho wa siku tufikie lengo la kuzalisha umeme wa kutosha utakaowezesha nchi yetu kuwa na viwanda vingi ili Tanzania ifikie uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Profesa Mdoe.
Aliongeza kuwa Wizara itatoa ushirikiano kwa wawekezaji mbalimbali wanaojitokeza kuwekeza katika Sekta za Nishati na Madini na ndio maana Waziri Muhongo kuanzia mwanzoni mwa mwezi wa Pili mwaka huu amefanya mazungumzo na makampuni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kusikiliza mapendekezo yao kuhusu uwekezaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo upepo, jua, maji, mawimbi ya bahari, makaa ya mawe, gesi asilia, bayogesi na joto ardhi ambapo kampuni zaidi ya 300 zilijitokeza.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Edenville, Cassiano Kaegele, alimshukuru Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi mbalimbali wanazofanya katika kuhakikisha kwamba miradi mbalimbali inatekelezwa na kueleza kuwa kasi iliyopo sasa ikiendelea miradi mingi itatekelezeka na Tanzania haitalazimika kununua umeme kutoka nchi nyingine kwani ina vyanzo vya kutosha vya kuzalisha umeme huo.
Naye Peet Meyer, Mjiolojia kutoka kampuni hiyo ameeleza kuwa uchimbaji wa makaa ya mawe katika maeneo hayo utafanyika kwa njia ya mgodi wa wazi (opencast) katika miaka kumi ya kwanza na baadaye watachimba chini ya ardhi na kwamba makadirio ya gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 176. Leseni hiyo ya uchimbaji ni ya miaka kumi na kampuni ya Edenville wanaweza kuihuisha tena baada ya miaka hiyo kupita.
No comments:
Post a Comment