HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 6, 2015

Madini kanda ya Kusini yashika kasi ukusanyaji maduhuli

Ofisa Madini , Kasuhu Warioba (wa pili kulia) akiwa katika banda la Wizara ya Nishati na Madini katika Maonesho ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi. Wa kwanza kulia ni Ephraim Mushi wa Kitengo cha Mazingira, Wizara ya Nishati na Madini.
Ofisa Madini , Kasuhu Warioba (kulia) akimwonesha madini ya vito, mwananchi (kushoto) aliyetembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini katika Maonesho ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.Mwenye shati la kijani ni Habbas Ngulilapi kutoka Idara ya Nishati, Wizara ya Nishati na Madini.
Kamishna Msaidizi wa Madini, kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka akiangalia vipeperushi mbalimbali mara alipotembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini katika Maonesho ya Wakulima (NaneNane) katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Na Teresia Mhagama

Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini-Mtwara imeendelea kufanya vizuri katika kutimiza malengo ya ukusanyaji maduhuli ya madini katika kanda hiyo na kufanikiwa kutimiza lengo kwa asilimia 102.86 katika mwaka wa fedha 2014/2015.

Hayo yameelezwa na Kasuhu Warioba, Ofisa Madini kutoka mkoani Mtwara wakati wa Maonesho ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi ambapo alieleza kuwa Kanda ya Kusini inajumuisha ofisi za madini za Mtwara na Nachingwea.


Alieleza kuwa Ofisi ya Madini Mtwara ilipewa lengo la kukusanya shilingi milioni Mia Tisa (900,000,000) lakini ilivuka lengo hilo na kukusanya zaidi ya shilingi milioni 925 (925,729,343.52) na kushika nafasi ya kwanza katika ukusanyaji maduhuli ya madini nchini katika mwaka 2014/2015.

" Ofisi ya Madini ya Nachingwea pia ilipewa lengo la makusanyo ya shilingi milioni Mia Tatu (300,000,000) lakini ofisi hiyo iliweza kukusanya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 159 (159,340,497) ambayo ni sawa na asilimia 53.11 katika kipindi cha nusu mwaka tu, kwani hii ni ofisi yetu mpya ambayo imeanzishwa ili kusogeza huduma karibu na wananchi" alisema Warioba.

Alieleza kuwa kwa ujumla Kanda ya Kusini ilipewa lengo la makusanyo la shilingi bilioni 1.2 (1,200,000,000) na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.85 (1,085, 069,840.52) ikiwa ni sawa na asilimia 90.42 na kuwa kanda ya kwanza ya madini kwa ukusanyaji maduhuli ya madini nchini.

"Katika mwaka huu wa fedha wa 2015/2016, Kanda ya Kusini tumepewa lengo la kukusanya shilingi bilioni Tatu (3,000,000,000) ambapo Ofisi ya Madini Mtwara inatakiwa kukusanya shilingi bilioni 2.4 (2,400,000,000) na ofisi ya madini ya Nachingwea inatakiwa kukusanya shilingi milioni Mia Sita (600,000,000)," alisema Warioba.

Alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na ofisi hiyo chini ya uongozi wa Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Benjamin Mchwampaka ambaye anahakikisha kwamba kunakuwa na utunzaji makini wa taarifa za ukusanyaji maduhuli jambo linalopelekea kuwa na rekodi sahihi za watu waliolipa na wasiolipa mrabaha katika kanda hiyo na hivyo kuleta ufanisi katika ufuatiliaji wa makusanyo.

Alieleza kuwa Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini pia imeweka kizuizi katika eneo la Nangurukulu mkoani Lindi ambacho huwawezesha maafisa madini kukagua magari yote yanayopitisha madini na hivyo kuweza kukusanya mrabaha unaostahili kulipwa serikalini.

"Endapo kuna mtu yeyote ataonekana kukwepa ulipaji mrabaha, Ofisi ya Madini huchukua jukumu la kumpa taarifa ya kutakiwa kulipa mrabaha kwa   wakati na endapo atakaidi agizo hilo, magari yao huzuiwa kusafirisha madini mpaka atakapolipa deni lake," alisema Warioba.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad