HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 3, 2015

Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wafurahishwa na huduma za matibabu ya madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa

Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wameelezea kufurahishwa kwao na huduma za matibabu zinazotolewa na madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.

Wakizungumza na mwandishi wetu aliyetembelea katika hospitali hiyo, mmoja wa wazee waliopata huduma ya matibabu ya ugonjwa wa moyo Bi. Salu Shinge amesema amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya moyo kwa muda mrefu lakini baada ya kuonana na Daktari bingwa siku ya Jumatatu na kuanza kutumia dawa, hali yake imbadilika na kwamba anajisikia nafuu kwa sasa.

" juzi nilikuwa naumwa sana, nilikuja hapa mwili ukiwa umevimba, nikamwona daktari akanipa dawa za siku tano, leo ni siku ya tatu, tayari nimeona mabadiliko makubwa. Nina imani nitapona, nawashukuru sana hawa waliotuletea madaktari."

Naye mama wa mtoto Faida Sayi amesema mtoto wake aliyekuwa anasumbuliwa na uvimbe shingoni kwa muda mrefu amepata huduma ya upasuaji na hivi sasa anaendelea vizuri.

"Uvimbe ulianza kama jipu lakini siku zilivyozidi kupita uvimbe haukuwa na usaha wowote kama ilivyo kawaida ya majipu. Tumehangaika na matibabu hadi kwa waganga hatukufanikiwa. Niliposikia kuna madaktari bingwa hapa nikamleta, wamempasua, saa anaendelea vizuri tu".

Hadi sasa jumla ya wagonjwa 450 wamepatiwa huduma za matibabu, ambao kati yao wagonjwa SABA wamefanyiwa upasuaji, wakiwemo watoto WATATU.

Huduma hizo za matibabu zitatolewa hospitalini hapo kwa muda wa siku tano kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa kwa ushirikiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wananchi wakisubiri kujiandikisha kwa ajili ya kupata namba za kuwaona madaktari bingwa wanaoendelea kutoa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Wananchi wakisubiri kuingia kwenye vyumba vya madaktari bingwa ili kupatiwa huduma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad