HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, April 19, 2015

TEMESA YATAKIWA KULIKABILI SOKO LA USHINDANI NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Mussa Iyombe amezungumzia umuhimu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kutangaza huduma wanazozitoa kwa wananchi ili jamii iweze kunufaika na huduma hizo kwa wakati na  gharama nafuu.

Akizungumza na Menejimenti ya TEMESA jijini Dar es salaam leo, Eng. Iyombe amesisitiza Wakala huo kuwa na wafanyakazi wenye weledi, waliokabidhiwa mamlaka kamili na wabunifu ili kuhuisha huduma zinazotolewa kwa wananchi na kujiongezea mapato.

“Hakikisheni mnatumia wataalamu mlionao kuleta tija kwa Wakala na kwa Serikali kwa ujumla ili mfikie malengo yenu na kuipunguzia Serikali mzigo wa kuwahudumia”, alisisitiza Eng. Iyombe. 

Aidha Eng. Iyombe ameagiza TEMESA kuimarisha uhusiano wake na jamii hasa sekta binafsi ili kubadili mtazamo uliopo sasa kuwa Wakala huo unatengeneza magari ya Serikali peke yake na hivyo kushindwa kuteka soko la sekta binafsi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) Eng. Marceline Magesa amemshukuru Katibu Mkuu kwa kuwapatia vifaa mbalimbali na mitambo na kuahidi kuwa vitatumika vizuri ili kuimarisha utendaji kazi wa TEMESA.

“Asilimia 100 ya mapato kwa baadhi ya mikoa tunayaacha mikoani ili kufufua mitambo iliyoko na kuboresha huduma za Ufundi, hivyo tumieni fursa hii kubuni miradi mingi ya kuongeza mapato”, amesema Eng. Magesa.

Ubunifu, kujitangaza na kutoa motisha kwa wafanyakazi inachangia ari ya kufanya kazi ambapo TEMESA mkoa wa Pwani na Tanga imeelezwa kufanya vizuri na hivyo kuhudumia taasisi mbalimbali binafsi na za umma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad