Na Abdulla Ali-Maelezo Zanzibar
Serikali ya Marekani imeamua kuwatembelea Vijana wa Bara la
Afrika kwa lengo la kukaa nao pamoja na kuzungumza nao juu ya
Changamoto na Matatizo yanayowakabili vijana hao.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje
wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Usalama wa Raia,
Demokrasia na Haki za Binadamu Bi. Sarah Sewall (pichani) wakati
akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya Kituo cha
Vijana iliyopo nyuma ya Kituo cha Polisi Madema, Wilaya ya
Mjini Unguja.
Amesema vijana wanakabiliwa na matatizo mengi kwa sasa
yanayowafanya kukata kabisa tamaa ya maisha na badala yake
kujiingiza katika vitendo viovu ikiwemo utumiaji wa madawa ya
kulevya, wizi, ujambazi na wengine kuweza kutumiwa na makundi
maovu yasiyo na tija kwao.
Aidha amesema kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ndio tatizo
kubwa zaidi duniani jambo ambalo lilimfanya Rais wa Marekani
Barack Obama wiki 3 zilizopita kuitisha mkutano wa pamoja wa
Dunia ili kujadili masuala ya vijana ambapo Taasisi Mbalimbali za
Kiserikali na Binafsi Duniani zilishiriki katika mkutano huo.
Amefahamisha kuwa lengo la ziara yake barani afrika ni
kuyaendeleza kwa kuyafikisha kwa vijana yale yote yaliyojadiliwa
katika mkutano huo ili kuwaonesha njia ya mafanikio vijana hao
pamoja na kuwapa msaada pindi utakapohitajika.
Akizungumzia kuhusiana na mauaji ya Watu Wenye Ulemavu
wa Ngozi (Albino) nchini Tanzania amesema Serikali yake
imeshachukua hatua mbalimbali katika kulinda haki za binadamu
duniani kote kwa kuwapatia ulinzi na usalama wakiwemo hao
albino ila juhudi zaidi za kuwalinda zinatakiwa kufanywa na
Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa albino wanakuwa
katika usalama zaidi.
Akigusia kuhusu mchakato wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika
mwaka huu nchini Tanzania amesema Serikali ya Marekani
imekuwa ikitoa msaada mkubwa kwa Serikali ya Tanzania wakati
wa uchaguzi hivyo itaendeleza na jitihada hizo ili kuhakikisha
uchaguzi unakuwa katika hali ya usalama na amani na kuepukana
na vurugu zisizo za lazima.
Nae Mwenyekiti Mtendaji wa Vituo vya Vijana Tanzania
Nd. Abdalla Miraji Othman amesema vituo vyao kwa sasa
vinakabiliwa na Changamoto nyingi ikiwemo usafiri pamoja na
posho na mishahara kwa wafanyakazi wa vituo hivyo kwani huwa
havitolewi kwa wakati jambo ambalo linarejesha nyuma kwa kiasi
kikubwa jitihada zao za kuwaokoa vijana kutokana na vitendo
viovu.
Akitoa wito wake Nd. Othman amesema ipo haja kwa Benki za
Kitanzania kupunguza masharti ya kutoa mikopo pamoja na Riba
ili vijana wamudu kuchukua mikopo katika Benki hizo kwa lengo
la kujiajiri na hatimae kujikomboa kimaisha.
Amesema Ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje
wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Usalama wa Raia,
Demokrasia na Haki za Binadamu Bi. Sarah Sewall ilikua ni ya
Siku 1 Visiwani Zanzibar ambapo ziara hiyo inatrajiwa kufanyika
takriban bara lote la Afrika kwa lengo la kukutana na vijana na
kuzungumza nao juu ya masuala mbalimbali.

.jpg)
No comments:
Post a Comment