Frank Mvungi-Maelezo
Serikali yaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 10,000 kwa ajili ya makazi ya wanajeshi kote nchini.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Meja Josephat Musira wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembelea eneo la Gongo la mboto jijini Dar es salaam ambapo sehemu ya mradi huo inatekelezwa.
“Lengo la ujenzi wa nyumba hizi ni kupunguza tatizo la muda mrefu la uhaba wa nyumba kwa ajili ya makazi ya Maafisa na askari wa Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa.”alisema Meja Musira.
Akifafanua Meja Musira amesema awamu ya kwanza ya mradi huo imeanza ambapo nyumba 6,064 zitajengwa na kugharimu dola za marekani milioni 300, utekelezaji wake unaendelea vizuri katika Mkoa wa Dar es salaam na Pwani tayari jumla ya nyumba 3128 zinajengwa.
Kwa Mkoa wa Dar es salaam Meja Musira amesema nyumba 2,228 zinajengwa katika maeneo ya Lugalo, Gongola mboto, Ukonga, Navy Kigamboni, Ubungo Kibangu, Kunduchi KTC, Mbweni JKT na Kimbiji.
Akieleza zaidi Meja Musira amesema nyumba 1,160 kwenye maeneo manne ya Lugalo na Gongolamboto umeshakamilika kwa asilimia 100 na ukaguzi na uhakiki umeshafanyika.
Kwa upande wa Mkoa wa Pwani Meja Musira alisema jumla ya nyumba 840 zinajengwa katika maeneo ya msangani,Nyumbu,Kiluvya, Kisarawe na shule ya mafunzo ya awali Kihangaiko.
Maeneo yanayohusika na mradi huu kwa sasa ni Arusha inatarajiwa kujengwa nyumba (792) Tanga (312) Pemba (320) Morogoro (616) Dodoma (592) Kagera (144) na Kigoma (160).
Kwa upande wake Mhandisi wa Wizara hiyo Bw. Stephen Mpapasingo amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu na unalenga kuondoa kabisa tataizo la makazi kwa Maafisa na askari wa Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa
Mkandarasi wa mradi huu ni kampuni ya Shaghai Construction (Group) General Company kutoka China.
Msemaji
wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Meja Josephat Musira
akiwaeleza Waandishi wa habari (Hawapo pichani)kuhusu Mradi wa ujenzi wa
Nyumba 10,000 kwa ajili ya makazi ya Wanajeshi ambapo kwa awamu ya
kwanza idadi ya nyumba 6064 zinatarajiwa kujengwa na mpaka sasa nyumba
1160 zimeshakamilika kwa ajili ya matumizi, wakati wa ziara ya waandishi
wa habari katika moja ya eneo la maradi Jijini Dar es Salaam. Kulia ni
Mkuu wa Kitengo cha Ushauri wa Majenzi wa Wizara hiyo Mhandisi Stephen
Mpapasingo.
Mkuu
wa Kitengo cha Ushauri wa Majenzi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Mhandisi Stephen Mpapasingo akiwaonesha waandishi wa
habari (hawapo pichani) sehemu ya jiko katika moja ya nyumba hizo.
Mkuu
wa Kitengo cha Ushauri wa Majenzi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Mhandisi Stephen Mpapasingo akiwaeleza Waandishi wa habari
(Hawapo pichani) kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi
wa ujenzi wa Nyumba 10,000 kwa ajili ya makazi ya Wanajeshi, wakati wa
ziara ya waandishi wa habari katika moja ya eneo la maradi Jijini Dar es
Salaam. Kushoto ni Msemaji wa Wizara hiyo Meja Josephat Musira


Baadhi
ya nyumba zilizojengwa eneo la Gongo la Mboto Jijini Dar es Salaam
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi Nyumba 10,000 kwa ajili ya
makazi ya Wanajeshi.Picha na Hassan Silayo.
No comments:
Post a Comment