Hatimaye Serikali imetimiza ahadi yake mapema leo mara baada ya Kivuko cha Mv. Kigamboni kuanza rasmi safari zake za usafirishaji.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Mussa Iyombe wakati akizindua kivuko hicho ambacho kilikuwa kikikarabatiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Wanamaji.
Mhandisi Iyombe amesema Kivuko hicho ambacho kinategemewa na wananchi walio wengi waishio Kigamboni na maeneo jirani kimeanza kutoa huduma zake za usafirishaji ambao ulikuwa umesitishwa kwa muda wa takribani mwezi mmoja.
“Ile ahadi ya kukikarabati na kukirudisha kivuko cha Mv. Kigamboni hatimaye leo imetimia na wananchi wamejionea wazi juu ya utendaji na ufatiliaji wa huduma muhimu kama hizi za vivuko”, alisema Katibu Mkuu Aidha, Katibu Mkuu amelipongeza Jeshi la Wananchi Tanzania Kikosi cha Wanamaji kwa uzalendo wao waliouonesha kwa kukamilisha ujenzi huo kwa gharama nafuu na kwa wakati ili kurejesha huduma za usafirishaji.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kigamboni Bw. Davis Hokororo ameipongeza Serikali kwa huduma ya ukarabati walioufanya na ameiomba serikali kuongeza kivuko kingine kikubwa ili kukidhi haja za wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani.
Pia ameiomba Serikali kutokupeleka kivuko cha Mv. Magogoni kwa wakati huu mpaka kusubiri kukamilika kwa barabara ya Kongowe ili kurahisisha huduma za usafirishaji kupitia njia ya vivuko na barabara.
Kivuko cha MV KIgamboni kikiwa majini kuelekea eneo la Ferry kwa ajili ya kuanza kutoa Huduma ya Usafiri.
Abiria wakipakia kwenye Kivuko cha MV Kigamboni mara baada ya kuanza kufanya kazi.
No comments:
Post a Comment