HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 31, 2014

TanTrade yapongezwa kwa kuboresha Muungano Kibiashara

Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa maonyesho ya biashara ya Eid El Fitri katika viwanja vya Maisara, wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Sabetha Mwambenja na katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi. Anna Bulondo.  
Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui akiangalia bidhaa za wajasiriamali kwenye maonyesho ya Biashara ya Eid El Fitri yanayofanyika katika viwanja vya Maisara, pamoja nae katika picha kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi. Anna Bulondo, na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Thawabay Kisasi.
Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko wa Zanzibar Nassor Mazrui akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Sabetha Mwambenja wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbali mbali wa serikali na TanTrade punde baada ya kufungua Maonesho ya Eid El Fitri visiwani humo. (Picha: Maelezo Zanzibar)

Waziri wa Viwanda, Masoko na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui ameipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, (Tantrade) kwa kuwa na utendaji unaozingatia Usawa kati ya Bara na Visiwani Zanzibar na kuboresha biashara pande zote.

Waziri Mazrui amesema hayo wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Maonesho ya Biashara ya Idd El Fitri yanayofanyika kwa siku nane Visiwani Zanzibar.

“Mimi kama waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya masoko viwanda na biashara katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nimeshuhudia utendaji mzuri ndani ya TanTrade unaozingatia usawa wa kibiashara kati ya Bara na Visiwani” alisema na kuongeza.

“Kupitia TanTrade wafanyabiashara wa hapa Zanzibar wanapata fursa ya kushiriki katika maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ambayo yanaandaliwa na Mamlaka hii bila ya kujali upande ambako maonesho haya yanaandaliwa, hili ni jambo jema na ni lakupongezwa kwani linakuza Uchumi wan chi na kutoa fursa sawa kwa wafanyabiashara, alisema Mazrui.

Waziri huyo aliongeza kwa kutoa wito kwa Wafanya Biashara wa ndani kuboresha bidhaa zao na kutumia fursa wanayo ipata katika maonesho mbalimbali wanayoshiriki kwa kujenga mahusiano ya kibiashara na mtandao utakao weza kuwaongezea mauzo ndani na nje ya nchi.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Sabetha Mwambenja amesema kuwa Tantrade itaendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara wa Tanzania na kuhakikisha Ubora na viwango vya bidhaa za Tanzania unaboresheka, huku akitanabaisha kuwa Mamlaka hiyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha Ofisi za kuduma Visiwai Zanzibar.

“Tunatambua umuhimu wa kuboresha na kupanua huduma zetu, hivyo tuliomba serikali itusaidie kupata jengo ambalo tungeweza kulitumia kama Ofisi za kudumu na tukapatiwa jengo hilo, na sasa tuko katika hatua za mwisho za kukamilisha ofisi zetu Visiwani Zanzibar” alisema.

“Ninaipongeza Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikiunga mkono jitihada zetu za kukuza biashara na uchumi wa Taifa kwa ujumla, tunawaahidi wafanyabiashara wote na Watanzania kwa ujumla kuwa TanTrade tutasimamia na kutoa fursa sawa kadri inavyowezekana.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade Bi. Anna Bulondo, pamoja na kutoa wito kwa Watanzania kujitokeza katika maonesho hayo ametoa wito kwa, taasisi za Serikali, mashirika binafsi na jumuiya ya wafanyabiashara kufanya maandalizi ya Maonesho ya Mapinduzi ya Zanzibar mapema ambayo yatafanyika kwa mara ya pili mjini Zanzibar.

“Naomba nitoe wito kwa taasisi mbalimbali za serikali, mashirika binafsi na wafanyabiashara kufanya maandalizi mapema ya maonesho ya Mapinduzi ambayo yatafanyika kwa mara ya pili visiwani Zanzibar baada ya kufanyika kwa mafanikio Makubwa mwaka jana wakati wa sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad