HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 8, 2013

Jiungeni na NHIF kwa huduma za Matibabu - Rais UTPC

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

RAIS wa Muungano wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Keneth Simbaya amewataka waandishi wa habari nchini kuweka mkakati wa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuondokana na hofu ya kukosa matibabu wakati wanapoumwa.

Rai hiyo ameitoa jijini Mwanza katika mkutano mkuu wa UTPC ambapo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulipata fursa ya kutoa mada kwa viongozi hao ya umhimu wa kujiunga na huduma zake hususan kwa waandishi wa habari.

“Ni wakati sasa wa kuangalia mnakwenda wapi…kujiwekea bima ya afya ni suala la msingi zaidi kwani gharama za matibabu ni kubwa na unaweza ukahitaji huduma hizo kipindi ambacho hauna fedha hivyo tafakarini vizuri na mfanye maamuzi ila kwa upande wangu nitakuwa wa kwanza kujiunga,” alisema.

Wakati akiwasilisha mada hiyo, Meneja Mwandamizi wa Uanachama, Celestine Muganga alisema kuwa huduma zinazotolewa na NHIF ni bora zaidi kwa kuwa zinampa uhuru mwanachama mwenyewe kuchagua mahali au kituo anachopenda kupata huduma hiyio.

Alisema mpaka sasa NHIF imesajili jumla ya vituo na maduka ya dawa 5,840 kwa nchi nzima hali inayorahisisha zaidi upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wanachama.

“Huduma za NHIF ni nzuri na zimeenea kila mahali hivyo mkijiunga mtanufaika zaidi ninyi pamoja na wategemezi wenu lakini pia kuondokana na mzigo na hofu ya kukosa matibabu pale mnapoumwa,” alisema Muganga.

Alisema kuwa pamoja na changamoto za hapa na pale zinazoukabili Mfuko kwa sasa ikiwemo kupanda kwa bei za dawa na huduma za matibabu, uwasilishaji wa madai ya kughushi unaofanywa na baadhi ya watoa huduma, Mfuko umeendelea kujipanga na kukabiliana na changamoto hizo.

Wakichangia mada hiyo baadhi ya washiriki wa mkutano huo, walisema kuwa NHIF imekuwa msaada mkubwa  Watanzania hivyo umuhimu wa wao kujiunga unazidi kuwa mkubwa zaidi.

Aidha waliuomba Mfuko kuangalia utaratibu wa namna waandishi wa habari watavyoweza kuchangia na hatimaye kuwa wanachama wake.

Akihitimisha suala hilo Makamu wa Rais wa UTPC, Jane Mihanji aliwataka viongozi wa vyama vya waandishi kwa ngazi ya Mkoa kujipanga kwa kuweka mikakati mizuri ya namna ya kujiunga na NHIF na mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii.
Meneja Mwandamizi wa Uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Celestine Muganga akitoa mada katika Mkutano Mkuu wa Muungano wa Vyama vya waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Abubakar Karsan akimkaribisha mtoa mada kutoka NHIF.
Washiriki wa mkutano Mkuu wa UTPC wakifuatilia mada ya NHIF iliyohusu umuhimu wa kujiunga na Mfuko huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad