Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza na Balozi wa Norway nchini Tanzania Ingunn Klepsvik. Balozi Klepsvik alifika Ofisini kwa Waziri Oktoba 3, 2013, kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kufuatia makubaliano yaliyofanyika nchini Norway hivi karibuni ya ushirikiano baina ya Mikoa hiyo na Miji ya Hammerfest na Sandnessjoen iliyoko Norway, ambayo uchumi wake umekua kutokana na wananchi wake kuzitumia fursa za uwepo wa rasilimali za mafuta na gesi asilia katika Miji yao.
Mameya wa Miji ya Mtwara na Lindi pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji hiyo wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye suti-katikati), alipokuwa akifafanua jambo wakati walipokutana na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ingunn Klepsvik, (kulia kwa waziri). Viongozi hao walikutana Ofisini kwa Waziri, jijini Dar es Salaam, Oktoba 23, 2013 ikiwa ni hatua ya awali ya kuanzisha ushirikiano baina ya Mikoa ya Kusini na Miji ya Hammerfest na Sandnessjoen ya nchini Norway.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Lindi, Mathei Makwinya (wa kwanza-kushoto), akifafanua jambo wakati wa Kikao baina ya Mameya wa Miji ya Mtwara na Lindi, Wenyeviti wa Halmashauri za Miji Hiyo na Balozi wa Norway nchini, Ingunn Klepsvik (wa pili-kutoka kulia). Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa kwanza kulia) ndiye alikuwa Mwenyeji wa Kikao hicho kilichojadili uwezekano wa kuanzisha ushirikiano baina ya Mikoa hiyo ya Kusini na Miji ya Hammerfest na Sandnessjoen ya Norway.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) na Balozi wa Norway nchini, Ingunn Klepsvik (kushoto kwa waziri) katika picha ya pamoja na Mameya wa Miji ya Mtwara na Lindi na Wenyeviti wa Halmshauri za Miji hiyo, mara baada ya kikao chao kilichojadili hatua za mwanzo za ushirikiano baina ya Mikoa ya Kusini na Miji ya Hammerfest na Sandnessjoen ya nchini Norway. Ushirikiano huo umelenga kuzitumia fursa za kiuchumi zilizopo katika Mikoa husika hususan rasilimali ya gesi asilia ili kuwaletea wananchi wake maendeleo na kukuza uchumi wake. Kikao hicho kilifanyika Oktoba 3, 2013 Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Na Hendrick Msangi
Ujumbe kutoka Norway unatarajiwa kutembelea nchini mapema mwezi Januari mwakani kwa lengo la kukutana na wananchi wa Mikoa ya Kusini na kujionea fursa za kiuchumi zinazopatikana katika Mikoa hiyo.
Ujio huo wa Wa-Norway umepangwa kufanyika kutokana na makubaliano baina ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mameya wa Miji ya Hammerfest na Sandnessjoen ya nchini Norway ya ushirikiano baina ya Miji hiyo na Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Katika Kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini Oktoba 3 mwaka huu, iliafikiwa kuwa pande zote mbili yaani Wawakilishi kutoka Norway na wale wa Mikoa ya Lindi na Mtwara watembeleane ili kila upande upate fursa kujionea kwa macho fursa zilizopo kila upande ili hatua hiyo iwasaidie kufikia makubaliano katika vipaumbele vitakavyofaa kwa pande hizo kushirikiana.
Aidha, katika Kikao hicho kilichowakutanisha pamoja Mameya wa Miji ya Lindi na Mtwara, Wenyeviti wa Halmashauri za Miji hiyo, Balozi wa Norway hapa nchini Ingunn Klepsivik na Mwenyeji wao Profesa Muhongo, ilikubalika kuwa Wa-Norway ndiyo waanze kuja Tanzania na baadaye Wawakilishi kutoka Lindi na Mtwara nao waende Norway ili kujionea maendeleo yaliyofikiwa na Miji husika kutokana na kuzitumia vema fursa za kiuchumi zilizopatikana kufuatia uwepo wa rasimali za gesi na mafuta.
Balozi Klepsivik alisifu makubaliano ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili na kusema yatakuwa yenye manufaa makubwa na yatawasaidia wananchi wa Mikoa ya Kusini kukua kiuchumi na hivyo kujiletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
“Serikali ya Norway iko tayari kuwasaidia wananchi wa Lindi na Mtwara kwa kuwaelimisha na kuwashauri kuhusu namna bora ya kuitumia fursa ya upatikanaji wa gesi asilia katika Mikoa yao ili kukuza kipato chao na kujiletea maendeleo,” alisema Mheshimiwa Balozi.
Naye Waziri Muhongo aliwasisitiza Viongozi kutoka Mtwara kuanza maandalizi mara moja kwa ajili ya kuupokea ugeni huo hapo Januari mwakani. “Haitapendeza waje hapa wakute hamjajiandaa, hakuna kitu cha kuwaonesha,” alisisitiza.
Kwa upande wao, viongozi kutoka Mikoa ya Kusini walioshiriki kikao hicho walimshukuru Waziri Muhongo kwa jitihada zake katika kuhakikisha wananchi wa Mikoa hiyo wananufaika na rasilimali ya gesi asilia iliyopo katika Mikoa yao. “Tunakiri kuwa tumeitambua nia yako njema ya kutaka tunufaike na rasilimali hii,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Lindi, Mathei Makwinya kwa niaba ya wenzake.

No comments:
Post a Comment