WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya zao kabla ya kuugua pamoja na kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili wanufaike na huduma zake.
Rai hiyo aliitoa Dar es Salaam juzi katika banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao uliendesha zoezi la upimaji wa afya za wananchi bure katika maonesho ya Tanzania Homes Expo.
“Ni vyema kwa kila mtanzania anapopata fursa kama hii akaitumia ili kujua afya yake hususan nyie wanahabari ambao ndio mmekuwa mstari wa mbele kuzifahamu hizi fursa, mtu ukijua afya yako ni rahisi kujikinga na magonjwa mengine hasa yasiyoambukizwa” alisema Prof. Mbarawa.
Waziri huyo ambaye naye alitumia fursa hiyo kupima afya yake na kupata ushauri wa kiafya kwa watalaam, aliupongeza Mfuko wa juhudi mbalimbali ambazo umekuwa ukifanya katika kutoa na kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.
Katika maonesho hayo ya siku mbili wananchi wengi wamepata huduma ya kupima afya zao na kupata ushauri ambao unalenga kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekuwa ukiendesha upimaji wa afya katika maeneo mbalimbali unaoambatana na utoaji elimu ya kujiunga na Mfuko huo pamoja na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) mifuko ambayo inapunguza mzigo mkubwa wa kugharamia matibabu kwa wananchi ambao wamejiunga nao.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja Masoko wa Mfuko huo, Angela Mziray aliwataka watanzania kujiunga na NHIF ili wanufaike na mafao yake likiwemo fao la wastaafu ambao wanatibiwa bure kwa maisha yao yote.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa akipima urefu katika banda la NHIF katika maonesho ya Tanzania Homes Expo yanayofanyika Mlimani City Dar es Salaam.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa akisaini kitabu cha wageni katika banda hilo baada ya kupima afya yake.
Wananchi mbalimbali wakiwa katika banda hilo kwa lengo la kupima na kupata elimu ya Mfuko huo.




No comments:
Post a Comment