HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 24, 2013

Makatibu Mahsusi Nishati na Madini waaswa kuwa waadilifu

 Mwenyekiti wa Umoja wa Makatibu Mahsusi  wa Wizara ya Nishati na Madini (TAPSEA) Marcelina Mushumbusi (katikati) akizungumza na watumishi wa Kada husika katika maadhimisho ya Siku ya Makatibu Mahsusi Tanzania, Agosti 23, 2013.  Maadhimisho hayo yalifanyika Makao Makuu ya Wizara, Dar es Salaam.
 Makatibu Mahsusi wa Wizara ya Nishati na Madini wakijadili mafanikio na changamoto ambazo wanazipata katika utendaji wao wa kazi, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Makatibu Mahsusi Tanzania.
Makatibu Mahsusi wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwa katika picha ya pamoja, walipokutana kuadhimisha Siku ya Makatibu Mahsusi Tanzania.
Baadhi ya Makatibu Mahsusi wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwa katika picha ya pamoja, walipokutana kuadhimisha Siku ya Makatibu Mahsusi Tanzania.

Na George Mremi na 
Hendrick Msangi

Mwenyekiti wa Umoja wa Makatibu Mahsusi  wa Wizara ya Nishati na Madini (TAPSEA) Marcelina Mushumbusi amewataka watumishi wa Kada hiyo katika Wizara husika kufanya kazi kwa uadilifu ili kujenga uaminifu kwa mwajiri wao, Serikali na jamii nzima.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Makatibu Mahsusi Tanzania yaliyofanyika Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam, Mushumbusi aliwasisitiza Makatibu Mahsusi hao kutoa huduma kwa weledi na kuwataka kuwa na upendo, umoja, na kusaidiana ili kufanikisha majukumu yao ya kila siku.

Wakiadhimisha siku hiyo muhimu, Makatibu Mahsusi wa Wizara ya Nishati na Madini walikutana pamoja kujadili mafanikio na changamoto ambazo wanazipata katika utendaji wao wa kazi.

Mushumbusi alitumia fursa hiyo kuomba Uongozi wa Wizara kutoa mafunzo ya weledi na maadili bora ya kazi kwa watumishi wa Kada hiyo.
Aidha, alishauri watumishi wengine wote wa Wizara wapewe mafunzo ya aina hiyo kulingana na taaluma zao ili kuboresha utendaji wa kazi za serikali kwa manufaa ya Watanzania wote.

Mwenyekiti huyo alimpongeza Katibu Mkuu wa Wizara Bw. Eliakim Maswi kwa kutoa fursa ya wao kujiendeleza kielimu  hali ambayo inawasaidia kuwa na ufanisi katika utendaji wao wa kazi.

Aliwataka Makatibu Mahsusi kuchangamkia fursa hiyo ya elimu kwa kuongeza ujuzi katika fani yao na pia aliwapa changamoto kusoma fani nyingine ambazo zitawasaidia kuendana na mabadiliko yanayotokana na kukua kwa teknolojia duniani kote.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad