HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 1, 2013

wanaochimba dawa (kujisaidia) hovyo wilaya ya Makete kukiona

Ofisi ya afya wilaya ya Makete mkoani Njombe imekusudia kununua kamera kwa ajili ya kupigia picha za baadhi ya watu wanaojisaidia ovyo mitaani kwa lengo la kuwadhibiti na kuwachukulia sheria watu wa namna hiyo ikiwemo kuwafikisha mahakamani

Kauli hiyo imetolewa leo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Makete na Afisa afya wilaya hiyo Bw. Boniphace Sanga katika kikao kilichowahusisha mkuu wa polisi Makete, Afisa biashara, afisa afya pamoja na wamiliki na wahudumu wa baa na vilabu vya pombe za kienyeji

Bw. Sanga amesema ofisi yake imefikia hatua hiyo baada ya kuona vitendo vya kujisaidia hovyo hasa maeneo ya baa na vilabu yanakithiri licha ya adhabu mbalimbali kuchukuliwa dhidi yao, na wengine kudai kuwa wanaonewa na ofisi yake, hivyo wameamua kununua kamera ambazo wakiwapiga picha watu hao picha moja wanawapelekea wenyewe na nyingine wanaihifadhi na kuitumia kama ushahidi mahakamani

Amesisitiza wamiliki na wahudumu hao kuhakikisha wanatunza usafi wa maeneo yao ya biashara kwa kuweka vyombo vya kuhifadhi taka na kuhakikisha wanapokwenda kuzitupa dampo vyombo hivyo wanarudi navyo, na kuwepo kwa maji moto ya kuoshea glasi ama vikombe vya kupimia pombe za kienyeji

Ameongeza vitu vingine wanavyotakiwa kuvifanya kuwa ni kuvaa sare sketi nyeusi, blauzi nyeupe na kofia ama kilemba na wanaume suruali nyeusi, shati nyeupe na kofia pamoja na kufunga taa za mwanga mkubwa kwenye maeneo ya giza ya nyumba zote za biashara za vileo kwani wateja wakishakunywa pombe hupenda kwenda jirani kwenye maeneo yenye giza na kujisaidia hapo

“Hayo ni maagizo tafadhali yazingatiwe la sivyo tutawanyang’anya leseni za kufanyia biashara, mteja akiona kagiza kadogo tuu hapo hapo anajisaidia na matokeo yake athari za mikojo ama vinyesi vinawaathiri watu wote” alisema Sanga

Kwa upande wake mkuu wa polisi wilaya ya Makete (OCD) SP Peter Kaiza amewataka wahudumu hao kuzingatia muda wa kufunga na kufungua nyumba za kuuzia vileo na kusisitiza kuwa hakuna mtu yeyoteakiwemo yeye ambaye upo juu ya sheria.

Amesema kumekuwa na utaratibu ambao unafanywa na baadhi ya maafisa wakubwa wa serikali ambao kwa wadhifa wao ama vyeo vyao huwafuata wahudumu wa vilabu ama baa na kuwataka kufungua kabla ya muda halali kwa kisingizio kwamba hakuna atakayekuuliza, hivyo kuwataka wakatae na kuwataka wawaambie waje muda wa kufungua ukifika

SP Kaiza amesema hali hiyo kwa hivi sasa haitafumbiwa macho na wao kama jeshi la polisi wataanza kuwakamata wote wanaokiuka masharti ya leseni zao na kuwafikisha mahakamani ili waadhibiwe kwa mujibu wa sheria

“Hakuna hata mmoja aliyepo juu ya sheria, na endapo tutakukamata umewahi kufungua ama umechelewa kufunga kwa kisingizio cha kuwahofia wateja wako kuwa ni watu wakubwa hapa, tutakumata na kukufikisha mahakamani, na kumbuka hakuna atakayekutetea na waliokudanganya watakuacha utaabike peke yako” alisema Kaiza

Naye Afisa biashara Bw. Edonia Mahenge amesema ni marufuku kuchangaya pombe za kienyeji na za viwandani na kuziuza katika chumba kimoja na kama mtu anataka kufanya hivyo anatakiwa kutenga mabanda mawili kwa kuwa hizo ni biashara nyingi tofauti

Amesema hayo kufuatia ombi lililotolewa na mmoja ya mmiliki wa kilabu cha pombe za kienyeji katika kitongoji cha Dombwela Bw. Harun ambaye amesema wanaomba kuruhisiwa kuuza vileo vyote kwa pamoja kwa kuwa hawana mitaji ya kutosha kupanga mabanda mawili, hali iliyopingwa na SP Kaiza na kusisitizwa na afisa biashara kuwa hiyo haiwezekani

Afisa biashara huyo amesema maagizo hayo yaliyotolewa katika kikao hicho yatatumika wilaya nzima hivyo wafanyabiashara hao wanatakiwa kuyazingatia na kutekeleza maagizo hayo.

Imeandikwa na Edwin Moshi, Makete

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad