HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, April 12, 2013

MJI WA MAKETE WAKABILIWA NA TATIZO LA UHABA WA MAJI


Mamlaka ya maji Makete mjini imesema inazalisha maji mita za ujazo 1500 hadi 1700 kati ya mita za ujazo 4500 zinazotakiwa ikiwa ni pungufu ya mita za ujazo 2000-2300, jambo linalopelekea maji kuwa ya mgawo mara kwa mara

Akizungumza na ripota wetu ofisini kwake Meneja wa mamlaka ya maji makete mjini Bw. Yonas Ndomba amesema kutokana na upungufu huo wa maji wanalazimika kufanya mgawo wa maji ambao umekuwa ukisaidia wateja kupata maji, ingawa ni kwa zamu

Amesema ingawa suala hilo la mgawo wa maji limekuwa likiwakera wananchi lakini mamlaka yake imesema haina namna ya kufanya kwa sasa zaidi ya kutoa mgawo wa maji huku ufumbuzi wa tatizo hilo likiendelea

Akizungumzia suala la ukosefu wa maji hata kama mvua zinaendelea kunyesha wilayani humo, Bw. Ndomba amesema kutokana na udogo wa bomba linalotoa maji kwenye chanzo hadi kwa watumiaji, hivyo haliwezi kubeba maji zaidi hata kama mvua zinanyesha na kujaza chanzo cha maji na badala yake maji yakijaa yanamwagikia chini

“Unajua mvua zikinyesha maji yanakuwa mengi sawa lakini kutokana na udogo wa bomba la kutoa maji kwenye chanzo kuja huku ni dogo kwani nila inchi 6, na badala yake linatakiwa bomba la inchi 8 ambalo litasaidia kupitisha maji mengi kwa wakati mmoja na matokeo yake hata mgawo wa maji utapungua kwa kuwa maji yanayopita ni mengi” Alisema Ndomba

Katika hatua nyingine meneja huyo ametaja hatua zinazochukuliwa na mamlaka yake kutatua tatizo hilo kuwa, tayari wameshaiandikia wizara ya maji kutenga fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuweka mabomba mapya ya inchi 8 kwenye chanzo cha maji cha Kidwiva ili maji yaongezeke zaidi ya sasa, na wizara imekubali na kinachosubiriwa ni fedha

Sanjari na hilo tayari mchakato wa kujenga chanzo cha maji katika mto mkubwa wa Luvanyila utakaogharimu zaidi ya bilioni 400 umeanza na upo kwenye hatua nzuri, na kinachosubiriwa hifi sasa ni fedha hizo kupatikana kutoka kwa wafadhili ili kazi hiyo ianze ambayo itamaliza changamoto za maji makete mjini

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad