Balozi Ramadhani Mwinyi,Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza wakati wa Mkutano wa Kamati Maalum inayohusika na Operesheni za Ulinzi wa Amani C-34. Wakati wa mkutano huo Mkuu wa Idara ya Operesheni ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa (DPKO), Bw. Herve Ladsous aliwataarifu washiriki wa mkutano huo, kwamba Idara hiyo ilikuwa ikijielekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa ( Unmanned Aerial System ) maarufu kama Drones katika operesheni za kulinda amani na kwamba teknolojia hiyo itafanyiwa majaribio katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC)
Na Mwandishi Maalum
Wakati Idara ya Operesheni ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa (DPKO) ikijielekeza katika matumizi ya teknolojiza za kisasa katika shughuli za ulinzi wa amani, zikiwamo ndege zisizokuwa na rubani (Unmanned Aerial Systems ) maarufu kama Drones. Baadhi ya mataifa hasa yale yanayoendelea yanataka kuwapo kwa majadiliano zaidi kuhusu matumizi ya zana hizo.
Taarifa ya matumizi ya teknolojia za kisasa katika ulinzi wa amani, imetolewa na Mkuu wa DPKO , Bw Herve Ladsous, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kamati Maalumu inayohusika na masuala ya operesheni za kulinda amani maarufu kama C-34. Kamati hiyo maalumu ipo chini ya Kamati ya Nne ya Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa yake, Bw Ladsous ameeleza kwamba uamuzi wa kutumia teknolojia za kisasa zikiwamo unmanned aerial systems (UAS) unalenga katika kuboresha utendaji kazi wa misheni za kulinda amani, kukusanya taarifa na kutoa tahadhari za awali na kubwa zaidi kuokoa maisha ya walinzi wa amani dhidi ya hujuma mbalimbali.
Katika mwaka uliopitia (2012) walinzi wa amani 111 wakiwamo watanzania sita wamepoteza maisha kwa nyakati tofauti kwa kushambuliwa wakati wakitekeleza majukumu yao ya kuwalinda wananchi katika nchi zenye migogoro.
Akieleza zaidi kuhusu mpango huo, Bw. Ladsous amesema, zana hizo zitaanza kwa majaribio katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kupitia misheni ya kutuliza amani MONUSCO.
“Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametoa pendekezo la kutumika kwa majaribio teknolojia hii katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tunafanya kazi kwa karibu na Baraza Kuu la Usalama , nchi mwenyeji, na wadau wengine kuhakikisha kwamba walinzi wetu wa amani wanapata fursa ya kutumia teknolojia ya kisasa” akasema Mkuu wa DPKO.
Na kuongeza kwamba matumizi ya teknolojia hizo ni muhimu si katika kuwalinda walinzi wa amani bali pia kuzijengea uwezo na maarifa misheni hizo.
Mkuu huyo wa DPKO akaeleza zaidi kwamba mchakato umeanza wa kuomba ridhaa kwa nchi mwenyeji, kuzijulisha nchi jirani, mawasiliano na nchi zinazotoa walinzi wa amani (TCC) na kuwauliza wauzaji wa zana hizo wale ambao wataonyesha nia.
Baadhi ya mataifa yaliyoendelea ingawa yanakili kwamba bado kuna hali ya sintofahamu na hofu kuhusiana na suala hilo,yanaunga mkono matumizi hayo katika kile wanachoamini kutasaidia sana kupunguza vifo vya walinzi wa amani.
Hata hivyo baadhi ya nchi zinazoendelea na ambazo zinachangia walinzi wa amani maarufu kama TCC, zinasisitiza kwamba uamuzi wa matumizi ya zana hizo za kisasa ni lazima yajadiliwe miongoni mwao . Ikiwa ni pamoja suala la sheria na sera za matumizi ya zana hizo, raslimali fedha na teknolojia inayoambatana na zana hizo.
Mkutano huu wa Kamati Maalum ya operesheni za kulinda amani licha ya kujadili suala zima la shughuli za ulinzi wa amani, unajadili pamoja na mambo mengine changamoto mbalimbali zinazowakabili walinzi wa amani na mfumo mzima wa utekelezaji wa operesheni hizo.
Baadhi yachangamoto zinazojadiliwa ni pamoja na mkanganyiko wa dhamana wanayobeba walinzi wa amani , uhaba na ufinyu wa raslimali fedha na vifaa, dhana ya ulinzi wa raia, ushirikishwaji katika utoaji wa maamuzi , ushiriki wa wanawake hususani Polisi wanawake katika ulinzi wa amani na mafunzo kwa walinzi hao wakiwamo pia Polisi, Magereza na Raia.
Suala la malipo kwa walinzi wa amani ni jambo ambalo pia limeendelea kutiliwa mkazo katika mkutano huu, na karibu wazungumuzaji wote ikiwambo Tanzania ambayo iliwakilishwa na Balozi Ramadhani Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Matifa.
Wazungumzaji wote wametaka na kusisitiza kwamba ni matumaini yao kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Kundi la Washauri kuhusu malipo ya walinzi wa amani pamoja na vifaa yatafanyiwa kazi ipasavyo wakati Kamati ya Tano ya baraza Kuu la Umoja wa Mataifa itakapokutana mwezi March mwaka huu.
No comments:
Post a Comment