Mtaa Kwa Mtaa Blog

KIPIMO CHA UTU WETU: UMESHAWAHI KUMUONA MTU HUYU?

Kama unaishi jijini Dar-es-salaam na hususani kama unatumia njia inayojulikana kama “Mbezi ya Chini” naamini kwamba umeshawahi kumuona mtu huyo anayeonekana katika picha hapo juu. Kwa muda mrefu sasa (yaweza kuwa miaka sasa) makazi yake yamekuwa hapo pembeni tu mwa daraja la Mlalakuwa karibu kabisa na yalipo makao makuu ya Jeshi La Kujenga Taifa (JKT) na pia karibu na yalipo mashirika mbalimbali yenye mlengo wa kijamii kama vile Red Cross nk.

Kutokana na jinsi eneo hilo lilivyo maarufu kwa foleni takribani kila jicho linalopita pale linamuona. Hujawahi kumuona? Kweli? Askari Polisi (wa traffic police na wa kawaida) wanaokuwepo eneo lile mara kwa mara wanamuona na wakati mwingine hata kupiga naye story mbili tatu. Nimewahi kushuhudia lundo la askari polisi wakisimamisha magari na pikipiki pale pale huku jamaa akiwa kakaa tu pale kimya akiangalia zoezi linaloendelea bila kuwabughudhi.

Njia ya Mbezi ya Chini hutumiwa pia na lundo la “viongozi” wa nchi hii wanaoishi maeneo ya Mbezi wanapita pale na kumuona. Wao pia, kama mimi na wewe, wanamuona.Wanapotupa jicho pale wanamtizama na kuendelea na safari zao.

Wahusika wa masuala ya afya, haki sawa, ustawi wa jamii nk. wanapita pale asubuhi wakielekea kwenye “ofisi” zao zinazoshughulikia masuala hayo na jioni wanarejea kutoka katika “ofisi” hizo na wanapita pale kuelekea majumbani mwao na kumuacha pale pale!

Mahali pale ambapo mtu huyu ambaye ni wazi anaonekana kuwa na matatizo ya akili (mental health issues) ameamua kuishi ni jalalani. Ni pachafu na pasipotamanika. Kimsingi mazingira anayoishi huyu bwana hayafai kwa mwanadamu kuishi. Isitoshe, pembeni yake tu, kuna mto ambao umegeuzwa kuwa dampo la takataka. Karibuni kutwa nzima huyu bwana hushinda amelala au ameketi katika kijigodoro kidogo na chakavu ambacho nimeambiwa alitupiwa na watu waliokuwa wamelitumia kumpeleka mgonjwa fulani hospitalini.

Sasa nimewahi kusoma na kusikia mahali kadhaa kwamba ukitaka kujua undani wa jamii fulani tizama jinsi inavyowashughulikia watu hawa katika jamii zao; wanawake, watoto na watu wenye matatizo ya akili (mental health issues). Sote tunajua jinsi gani jamii yetu inashughulikia au kutoshughulikia masuala ya wanawake. Tunatambua fika jinsi tunavyojali au kutowajali watoto (ajira kwa watoto, watoto wa mitaani nk vinaweza kukupa majibu ya haraka). Pia sasa,na mfano ulio mbele yetu, twaweza tambua ni jinsi gani tunawajali au kutowajali wenzetu wanaokumbwa na matatizo ya akili. Picha ya jamii yetu?

Sina uhakika na sera yetu ya taifa ya namna ya kushughulikia watu wenye matatizo kama anayoonekana kuwa nayo huyu bwana lakini ni wazi kwamba hastahili kuwa pale. Mbaya zaidi ni kwamba huyu yupo mahali pa wazi. Mahali ambapo kama nilivyogusia hapo juu, naamini wahusika wa moja kwa moja wanamuona kila siku na kuamua kwa makusudi kumpotezea tu. Vipi kuhusu wale ambao wapo huko walipo na ambao hawaonekani?

Unaweza kujiuliza kwamba ndugu mwandishi, mbona wewe huendi basi na kumuondoa pale? Ni kweli na swali lako litakuwa na mantiki. Pamoja na hayo, utetezi wangu utakuwa kwamba sina utaalamu wowote wa kushughulikia watu wenye matatizo ya akili(naamini kwa dhati kwamba huyu mwenzetu ana matatizo hayo). Wapo wataalamu waliosomea na wenye uwezo zaidi wa kumsaidia.

Nimeandika hapa kama kutoa wito. Nipo tayari kusaidiana na yeyote mwenye utaalamu zaidi au wahusika wa moja kwa moja ambao naamini ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Mtu huyu ni sehemu ya jamii yetu. Kumsaidia ni kuwajibika na kuonyesha utu wetu. Kumuacha mtanzania mwenzetu (na watanzania wengine wengi) katika hali kama ile sio sawa. Kama jamii tunawajibika. Nakaribisha maoni na ushauri. Unaweza kutuma maoni hapa kwenye post hii au kutumia bongocelebrity at gmail dot com. Asante.

Post a Comment

KAMERA YA MTAA KWA MTAA

[KAMERA YA MTAA KWA MTAA][carousel2]

HABARI

[HABARI][fbig1]

SHEREHE

[HARUSI][gallery1]

MKCT

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget