Mkazi mmoja wa Kijiji cha Kiwira wilaya Rungwe mkoani Mbeya,alietambulika kwa jina la Joseph Mwaenga (32) ambae ni mwendesha pikipiki (Bodaboda) anusurika kujilipua na kukilipua kituo cha Polisi katika mji huo akipinga vitendo vya uonevu vinavyofanywa na askari Kituo hicho.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya,Diwani Athuman amethibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati akizungumza na wanahabari leo kuwa tukio hilo lilimetokea jana majira ya 5 usiku katika eneo la kituo hicho .
Alisema kuwa kijana huyo ambae ni mwendesha boda boda alifikishwa kituoni hapo baada ya kufanya vurugu katika kijiwe cha maegesho ya pikipiki na baada ya hapo alipokonywa pikipiki yake (Boda Boda ) na wananchi na kuifikisha polisi .
Hata hivyo baada ya kufikishwa kituoni hapo akiwa nje ya kituo alijimwagia petrol na kumwagia kituo cha polisi kisha kutoa kiberiti na kutaka kujilipua yeye na kituo hicho kabla ya kudhibitiwa na askari wa zamu.
Kamanda Athuman alisema kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kufanya vurugu kijiweni wananchi walimpokonya boda boda yake na kuipeleka kituo cha polisi na ndipo kijana huyo alipoamua kuifuata boda boda yake kituo cha polisi huku akiwa na dumu la mafuta ya Petrol na kiberiti na baada ya kufika nje ya kituo hicho alijimwagia mafuta mwili mzima na kumwagia kituo cha polisi na kisha kutaka kujitoa muhanga kwa kujilipua .
Alisema kuwa hakuna madhara yaliyojitokeza kwa binadamu wala mali juu ya tukio hilo na mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment