HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, November 18, 2012

JB Mpiana kuwasili nchini Novemba 26

Mkurugenzi wa QS Muhonda J Entertainment, Joseph Muhonda (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Millennium Business Park, Kijitonyama jijini Dar es Salaam mapema leo asubuhi wakati akizungumzia onyesho la Mwanamuziki wa Kimataifa kutoka nchini Congo,JB Mpiana kwa kushirikiana na Mashujaa Band litakalofanyika katika viwanja vya Leaders Novemba 30. Wengine kulia ni rais wa Mashujaa, Chaz Baba na kushoto ni Mshauri wa bendi, King Dodo.
MWANAMUZIKI nguli wa dansi Afrika, JB Mpiana anatarajiwa kuwasili nchini Novemba 26, mwaka huu kwa ajili ya kupamba uzinduzi wa albamu ya Mashujaa Band Novemba 30, mwaka huu katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam na baadaye katika mikoa ya Arusha Novemba 28 na Mwanza Desemba 2.

Akizungumza na Waandishi wa Habari asubuhi ya leo katika ukumbi wa Millennium Business Park, Kijitonyama, Dar es Salaam, rais wa bendi ya Mashujaa, Charles Gabriel Cyprian ‘Chaz Baba’, alisema mkali huyo wa dansi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) anakuja kundi lake zima la Wenge Musica BCBG.

JB Mpiana ambaye kwa sasa anatamba na albamu yake ya mpya iitwayo Biloko, anatarajiwa kupagawisha Watanzania na rap yake mpya iitwayo Amataka Na Punda yaani, Panda Punda, ambayo kwa Kongo inapendwa ile mbaya.

Chaz Baba alisema kwamba maandalizi ya onyesho lao yanaendela vizuri kwa ujumla na wanamuziki wapo tayari kuwapa raha Watanzania siku hiyo.

Chaz Baba alisema bendi yao itaingia kambini wiki ijayo nje kidogo ya Dar es Salaam, ambako hawataki kuweka wazi, ili kuwaepushia usumbufu wanamuziki wakati zoezi hilo gumu la maandalizi ya shoo ya kufa mtu.

Alisema albamu yao, wanayozindua iitwayo Risasi Kidole ina nyimbo sita, ambazo ni Risasi Kidole yenyewe utunzi wake Chaz Baba, Ungenieleza utunzi wake Raja Ladha, Umeninyima utunzi wa Freddy Masimango, Hukumu ya Mnafiki utunzi wake Jado FFU, Kwa Mkweo utunzi wake Baba Isaya na Penzi la Mvutano, ambao umetungwa na Masoud Namba ya Mwisho.

Chaz Baba alisema kama ilivyopangwa, mbali na JB Mpiana, wanamuziki wengine watakaopamba uzinduzi huo ni MB Dogg, H Baba, Ney wa Mitego na wengineo ambao watajulikana baadaye.

“Sisi kwa upande wetu tumejipanga vizuri kuwapa watu burudani ambayo tunajua kwa muda mrefu wameikosa, Mashujaa tunakuja kushujaa, ushujaa wa kuwaburudisha watu na kukata kabisa kiu yao,”alisema Chaz Baba.

Alisema wanataka kufanya shoo ambayo hata JB mwenyewe akiona atakubali kwamba Tanzania kuna bendi yenye ubora sawa na bendi za kwao, Kongo, ambayo ni Mashujaa.

“Hadi sasa wapenzi wa muziki hapa Dar es Salaam ambao wamebahatika kuona shoo zetu wanakiri sisi ndio mabingwa wapya wa muziki wa dansi Tanzania, sasa tunataka tumdhihirishie hilo na JB Mpiana,”alisema Chaz Baba.

Wakati onyesho la Dar es Salaam litafanyila Leaders, Mwanza itakuwa kwenye ukumbi wa Villa Park na Arusha ni Tripple A.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad