Sheikh
Ponda Issa Ponda, akifunguliwa pingu, baada ya kufikishwa kwenye chumba
cha mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana Alhamisi
Novemba 1, 2012.
Kiongozi huyo mwenye msimamo mkali, alifikishwa kwa mara ya pili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pamoja na wafuasi wake ambapo hakimu anayesikiliza kesi dhidi yake,
Victoria Nongwa, ya kuvamia eneo la Markaz, Chang'ombe jijini Dar es
Salaam, ambapo waliharibu na kuiba mali mbali mbali zenye thamani ya
shilingi milioni 59, madai ambayo washtakiwa wote waliyakanusha.
Hakimu huyo alikubali kutoa dhamana kwa washtakiwa wote isipokuwa
kiongozi huyo ambaye ni mshtakiwa namba 1 kwa madai kuwa bado Mkurugenzi
wa Mashtaka nchini (DPP), hajaondoa pingamizi lake la kuzuia dhamana
kwa mshtakiwa namba moja.
Ulinzi katika mahakama hiyo ulikuwa ni mkali na haujawahi kutokea katika miaka ya hivi
karibuni, ambapo pamoja na mambo mengine, palifungwa CCTV Cameras, vifaa
vya kugundua vitu vyenye asili ya chuma, polisi wa kutuliza ghasia magereza na wale wa FFU, polisi wa farasi na mbwa, pamoja na askari
kanzu waliotapakaa kila kona ya maeneo ya jirani na mahakama hiyo kubwa
jijini Dar es Salaam.
Kikundi kidogo cha wafuasi wa Sheikh Ponda, kilijaribu kuleta rabsha,
lakini polisi walitumia busara na kuwaelekeza kilichoamuliwa mahakamani
ambapo pamoja na kusuasua kuondoka eneo hilo la mahakama, lakini
hatimaye waliondoka huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwafuata kwa
nyuma hadi eneo la makutano ya barabara za Bibi Titi na ile ya Morogoro
nao wakatawanyika.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya habari, kulikuwepo taarifa kuwa
wafuasi hao walipanga kutega milipuko kwenye eneo la mahakama na pia
walisambaza vipeperushi vyenye vitisho kadhaa, ikiwa ni pamoja na
kufanya maandamano makubwa ya kulazimisha kiongozi huyo aachiliwe.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 15 mwaka huu itakapotajwa tena |
No comments:
Post a Comment