HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 24, 2012

NHC YAZINDUA UUZWAJI WA NYUMBA ZA MRADI WA UJENZI WA MINDU JIJINI DAR LEO

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa,David Shambwe (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati wa kuzindua rasmi mauzo ya nyumba katika mradi wake mpya wa Mindu,Upanga jijini Dar es Salaam.Wengine pichani toka kulia ni Meneja Mahusiano ya Jamii wa Shirika la Nyumba la Taifa,Muungano Saguya,Meneja Masoko na Utafiti wa Shirika la Nyumba la Taifa,Itandula Gambalagi na mwisho ni Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa Mkoa wa Upanga,Benedict Kilimba.
Meneja Masoko na Utafiti wa Shirika la Nyumba la Taifa,Itandula Gambalagi akiwaonyesha baadhi ya Waandishi wa Habari sehemu ya Mradi wa Jengo Jipya lililopo Mtaa wa Mindu,Upanga jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa,David Shambwe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kutembelea mradi wake mpya wa Mindu,Upanga jijini Dar es Salaam.

Kwa mara nyingine tena Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) leo 24 Oktoba, 2012 limezindua rasmi mauzo ya nyumba katika mradi wake mpya wa Mindu, jijini Dar es Salaam. 

Ujenzi wa mradi huu ulianza rasmi mwezi Novemba mwaka 2011, na unatarajiwa kukamilika rasmi Aprili 2013 na mteja kuweza kukabidhiwa nyumba yake mwezi Mei 2013, ikiwa ni miezi 18 baada ya kuanza ujenzi. Mradi unatarajiwa kugharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 11 mpaka utakapomalizika, fedha zinazogharamiwa na Shirika kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo fedha za mikopo ya benki. 

Mradi huu uliopo mtaa wa Mindu eneo la Upanga, takribani mita 100 kutoka Hospitali Kuu ya Taifa Muhimbili, una sehemu ya nyumba 60 za kuuzwa zilizopo kwenye majengo pacha ya ghorofa 15, uko sehemu zenye huduma zote muhimu za kijamii zikiwamo hospitali, shule, maduka, na masoko. Pia Mradi unatarajiwa kuboresha maisha ya wanunuzi wa nyumba hizi kwani upo karibu kabisa na katikati ya jiji na kwamba mnunuzi anaweza kwenda kazini bila kutumia gharama yoyote ya usafiri wa gari. 

Aidha, nyumba zipo ndani ya uzio kwa ajili ya usalama wa wakaazi wake na kuna maegesho ya magari ya kutosha. Nyumba 60 tu zinazouzwa ambapo kila nyumba ina vyumba vitatu vya kulala, vyo vinajitegemea. Kila nyumba ina ukubwa wa mita za mraba 141 (sq.m), sebule iliyoungana na eneo la kula chakula, choo cha umma, jiko kubwa la kisasa na eneo la kufulia na kuanikia nguo. 

Sifa za ziada za mradi huu ni kuwa na eneo maalum la kukusanyia taka, nyumba zote zina viyoyozi, vifaa vya kung’amua moto, sehemu iliyotengwa maalum kwa ajili ya kufanyia mazoezi (gym), bwawa la kuogelea (swimming pool) na eneo kubwa la ziada la maegesho ya magari. 

 Kila nyumba itauzwa kwa bei ya TZS 272,050,673.08 bila kodi ya ongezeko la thamani (VAT ) na TZS 321,019,794.24 ikiwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Tunawahamasisha na kuwakaribisha watanzania wote walio nchini na nje ya nchi kujitokeza ili kununua nyumba hizo. 

Wanaweza kufanya mawasiliano na Makao Makuu ya Shirika, Ofisi zetu za Mikoa au kupitia barua pepe na kukamilisha taratibu mapema kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye mchakato ulio wazi wa manunuzi. Katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba, Shirika linajenga nyumba za gharama ya juu, kati na chini ili kuwahudumia watanzania wa kada zote. 

Katika azma hiyo, nyumba 10,000 zitakazojengwa kufikia 2015 zitahusu watu wa kipato cha juu na nyumba 5,000 zitakazojengwa kufikia mwaka huo zitakuwa ni nyumba za watu wa kipato cha chini. 

Shirika limeanza kujenga nyumba za gharama ya kati na juu ili kupata faida itakayoliwezesha kuwajengea watu wa kipato cha chini nyumba za gharama nafuu. Hii inatokana na ukweli kuwa Shirika halipati ruzuku toka serikalini ya kujenga nyumba kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini. 

Mradi huu wa Mindu tunaouzindua hii leo, ni moja ya miradi ya ujenzi wa nyumba za watu wenye kipato cha juu.. Ukiwa mdau na mnunuzi mtarajiwa, ama una ndugu/rafiki anayetamani kununua nyumba katika mradi huu, wasiliana na Kitengo cha Mauzo simu namba 0754 444 333; barua pepe: sales@nhctz.com na pia tembelea tovuti ya Shirika www.nhctz.com kwa maelezo zaidi. 

Links:


 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad