Ndugu zangu,
Yanayotokea
katika nchi yetu kwa sasa yanatutaka tufikiri kwa bidii. Kama nchi kuna
safari tumeifunga. Na tulivyo Waafrika, tu mahodari wa kufunga safari,
lakini si mahodari wa kupanga safari. Kufunga na kupanga safari ni vitu
viwili tofauti.
Ndugu zangu,
Ni
vigumu leo kwa Wana wa Israel kuamua kurudi tena Misri, hata kama,
pamoja na chawa na kunguni walioaacha Misri, bado, kuna wanaokumbuka
samaki na masufuria ya pilau waliyoayaacha Misri.
Lakini, kijamii, na kwa kuingalia jamii yetu hii ilikotoka, ilipo sasa
na inakoelekea, na tuone sasa, kuwa hakuna ugumu wa kurudi tena Misri.
Na hapa nitazungumzia umuhimu wa sisi WaTanzania kujitambua.
Nahofia,
kuwa moja ya kiini ya haya yanayotukuta sasa ni dhambi ya Ubaguzi
iliyoanza kututafuna pole pole. Taratibu tunapoteza uwezo wetu wa
kujitambua. Ni ukweli sasa, kuwa Watanzania hatujitambui, na kibaya
zaidi, baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa na kidini wanapoonyesha wazi
wazi kuwa hawajitambui.
Maana, tumeanza sasa kuzungumza lugha za ' Wao Wakristo' na ' Sisi Waislamu'.
Tunasahau, kuwa sisi ni ndugu wa damu. Kuwa SISI ni Watanzania Kwanza.
Na lililo la kwanza kwetu ni ' Nchi Yetu' na maslahi yake.
Hii
ni Nchi Yetu Sote.
Kila Mtanzania kwa nafasi yake ana lazima ya kupigania Usalama wa Taifa
letu. Usalama wa Nchi Yetu tuliyozaliwa. Hatuwezi kuilinda na kuijenga
Nchi Yetu kwenye mazingira ya kubaguana. Kwenye mazingira ya kugawanyika
kwa misingi ya udini, ukabila na rangi.
Na hapa nitamrejea tena Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na dhana ya
Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa.
Ni
Mwalimu Nyerere aliyeuanzisha na kuusimamia mradi mkubwa wa Ujenzi wa
Umoja wa Kitaifa, hata hivyo, tunaona sasa unavyoporomoka na kuliacha
taifa letu mashakani. Ndio, Mwalimu alijenga misingi imara ya Ujenzi wa
Umoja Wa Kitaifa ( Nation Building).
Kuijenga
jamii ya Watanzania yenye kuamini kwenye ukweli kuwa sisi sote ni
ndugu. Kwamba Nchi yetu haina dini. Yenye kupiga vita ubaguzi wa aina
zote, iwe wa rangi, kabila au dini. Ilimchukua Mwalimu na taifa letu
miaka mingi sana kuijenga misingi hiyo iliyowawezesha pia Watanzania
kuwa na mioyo ya uzalendo kwa Taifa lao.
Tunaona
sasa, kazi hiyo iliyochukua miaka mingi, kutokana na ubinafsi na uroho
wa madaraka ya baadhi ya wanasiasa wetu, wanapelekea kubomoka kwa
misingi hiyo na kuliacha taifa letu kwenye hatari ya kuangamia.
Ndio,
msingi wake ni ubaguzi wa kisiasa unaotokana na ubinafsi na tamaa ya
mali kwa baadhi ya tuliowapa dhamana za kufanya maamuzi makubwa kwa
niaba yetu.
Ni hali ya baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi kuishiwa chembe chembe
za uzalendo; mapenzi kwa nchi yao.Ni watu wenye kulinda maslahi yao na
ya wanaowazunguka. Wako tayari hata kutumia mbinu za Umafia kutimiza
malengo yao. Kuna Watanzania wengi sasa wanaopoteza mioyo ya uzalendo
kwa nchi yao.
Kuna
hata wenye kufikia kutamka; 'Nchi hii ina wenyewe'. Kuna anayetamka
hilo kwa lengo la kumtishia mwenzake au kulazimisha kitu fulani
kifanyike. Lakini, kuna wenye kutamka hivyo kuashiria kukata tamaa. Kuwa
hata wafanye nini, hakuna anayewasikiliza ama kuwajali.
Hizi si dalili njema kwa taifa. Kuna wanaoiba mali ya umma mchana wa jua
kali. Hakuna anayewagusa.
Ukiuliza
utajibiwa; “Ah! Nchi ina wenyewe!”. Kwamba kuna baadhi yetu hawajisikii
kuguswa na nchi hii, hawajisikii kuwa na nguvu ya kupiga vita maovu
yanayotusumbua. Baadhi yetu wameanza kupungukiwa na mapenzi na nchi yao.
Juni
16, 2004 nilipata kuandika hili kwenye gazeti la Majira; kuwa Tanzania
ina vyote, kasoro Watanzania. Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri
sana. Ni nchi ya kujivunia. Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo.
Ni nchi yenye rasilimali nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa,
milima, mabonde, bahari na vivutio vingi vya asili.
Hata
hivyo, Tanzania ni moja ya nchi masikini sana duniani. Kwa nini? Ndio,
kikubwa kinachokosekana Tanzania ni Watanzania.
Tanzania tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa makundi mbali
mbali wenye kwenda kwa staili ya 'kila mtu na lwake'. Idadi ya
Watanzania wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua.
Ubinafsi umekithiri, na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na
viongozi.
Ndugu zangu,
Hakuna ugumu wa kurudi Misri. Tuna lazima ya kupanga safari ya kurudi tena Misri. Inawezekana.
Na hilo ni Neno la Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa,
No comments:
Post a Comment