Katika
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mahesabu za Mashirika ya UMMA (POAC) mnamo
tarehe 24/10/2012 Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt. Ramadhani K. Dau akijibu
maswali ya Waheshimiwa Wabunge alitoa maelezo ya msingi kuhusu umuhimu
na dhana kamili ya Hifadhi ya Jamii.
Katika
maelezo hayo alifafanua kuhusu madhara ya kujitoa kwenye mfuko kwa
mwanachama aliye na uwezo wa kuendelea na kazi, na alisisitiza kuwa
madhara ni kwa Mwanachama zaidi kuliko kwa Mfuko.
Dkt.Dau alifafanua kuwa uamuzi wa kusitisha kwa Mafao ya kujitoa hauna
uhusiano wowote na hali ya sasa ya kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii.
Dkt.
Dau aliieleza Kamati ya Bunge kuwa hali ya kifedha ya Mfuko wa Hifadhi
ya Jamii hupimwa kwa kufanya Actuarial Valuation. Kwa upande wa NSSF
zoezi hilo limefanywa mwaka 2009 na Kampuni kutoka Canada iliyoteuliwa
na ILO na mwaka 2010 na Kampuni kutoka Afrika Kusini iliyoteuliwa na
SSRA.
Matokeo
yameonyesha kuwa NSSF HAINA MATATIZO YA KIFEDHA kwa sababu ina uwezo wa
kuwalipa Wanachama wake na kulipia gharama za uendeshaji kwa kipindi
cha miaka 50 ijayo bila kutetereka.
Dkt.
Dau alifafanua zaidi kuhusu kutokuwepo kwa mafao ya kujitoa katika
mfumo mzima wa Pensheni ulimwenguni kwa muongozo wa Shirika la Kazi
Duniani (ILO) namba 102 wa mwaka 1952 [The ILO Social Security (Minimum
Standards) Convention, 1952 No. 102] ambao ndio unatoa maelekezo ya
jumla kuhusu Sekta ya Hifadhi ya Jamii ulimwenguni kote.
Katika
Muongozo huu ILO imetamka wazi kuwa kuna aina tisa (9) za mafao
yanayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na katika hayo hakuna mafao
ya kujitoa.
HITIMISHO
Tunapenda kuwataarifu Wanachama na Wananchi kwa ujumla kuwa majibu haya
ndio yaliyotolewa katika Kamati ya Bunge.
Taarifa
zilizotolewa na baadhi ya Vyombo vya Habari kuwa “Mkurugenzi Mkuu wa
NSSF apinga Mafao ya Kujitoa” zimetolewa nje ya maudhui yaani “Out of
Context”
Suala la Mafao ya kujitoa (Withdrawal Benefit) linashughulikiwa na
Serikali na iwapo itaamuliwa na Bunge kurudisha mafao hayo,
NSSF HAINA PINGAMIZI na uamuzi huo na italipa mafao hayo bila wasiwasi wowote kwani ina uwezo mkubwa wa kifedha.
IMETOLEWA NA IDARA YA UHUSIANO - NSSF
No comments:
Post a Comment