HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 23, 2012

Jeshi la polisi kuanza operation ya kukagua leseni feki za udereva

Na Jackline Swai, Arusha.

JESHI la polisi mkoani hapa kwa kushirikiana na kikosi cha usalama barabarani kimeanzisha operation maalumu ya kukagua madereva ambao hawana leseni mpya za udereva pamoja na vyeti vya kuonyesha vyuo vya udereva walivyosoma.

Hatua hiyo imekuja baada ya kugundulika kuwa asilimia kubwa ya madereva wana leseni mpya ambazo ni feki na wamezipata kwa njia ya panya bila kupitia shule mbalimbali za udereva na kupatiwa vyeti vya kuhitimu masomo hayo.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa kikosi cha usalama barabara mkoani Arusha,(RTO) ,Marison Mwakyembe wakati akizungumza ofisini kwake kuhusiana na hali halisi iliyo hivi sasa na kuwepo kwa wimbi kubwa sana la leseni feki zinazotolewa kwa madereva katika maeneo mbalimbali.

Alisema kuwa, walianzisha operation hiyo july 4 mwaka huu ambapo hadi sasa hivi wameweza kukamata jumla ya leseni feki 7 huku madereva wake wakiwa hawana vyeti vya kuhitimu chuo cha udereva , hali ambayo imepelekea jeshi la polisi kuwa makini zaidi kutokana na hali hiyo.

Alifafanua kuwa, operation hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa sana kupunguza wimbi kubwa la ajali zinazotokea kila siku kutokana na kutokuwa na madereva wasiojua sheria za barabara kutokana na kutopitia vyuo vya udereva na kupatiwa elimu hiyo.

Alisema kuwa, kufuatia hali hiyo madereva hayo walinyang’anywa leseni hizo feki na walipotakiwa kwenda kuleta cheti cha kuhitimu udereva hakuna hata mmoja aliyefanikiwa kupeleka ,hivyo aliwataka kwenda shule kusoma na kupata vyeti hivyo ndipo waweze kupatiwa leseni zinazohitajika na sio kupitia njia za panya.

Mwakyembe aliongeza kuwa, asilimia kubwa ya madereva wamekuwa wakipitia njia za panya kupata leseni hizo ,ambapo wengi wao wamekuwa wakitumia kiasi kikubwa cha fedha kuanzia 500,000 hadi 600,000 kupitia njia za panya ili kupata leseni mpya, ambapo amewaonya mara moja kuacha tabia hiyo kwani ni hasara kwao pamoja na kuwa na leseni lazima waende shule wakasome na wapate vyeti vya udereva.

‘Mimi nashangaa sana jamani madereva tunawaelimisha kila siku waende shule kusoma na kupewa cheti kwani gharama yenyewe ya kusoma ni 200,000 tu,na wanasoma kwa muda wa wiki mbili tu,lakini wanaishia kudanganywa na watu wa mitaani na kupoteza kiasi kikubwa sana cha fedha bila kujua kuwa wataingia gharama mara mbili, hivyo ni lazima dereva yoyote awe na cheti cha udereva na leseni yake’alisema Mwakyembe.

Alifafanua zaidi kuwa, katika operation hii wanayofanya hivi sasa kila dereva ni lazima aende shule kusoma na kupitia sheria zote za barabarani ,na atatakiwa kutembea na leseni katika gari lake sambamba na cheti chake cha shule aliyosoma , na hii ni ili kudhibiti hali ya leseni mpya feki ambazo zimeenea kwa kasi sana.

Aliongeza kuwa, ni lazima wamiliki wa magari kuhakikisha wanakuwa na sheria zao katika kuwakabithi magari madereva waliosoma na wenye vyeti badala ya kuridhika na leseni ambazo wanakuwa nazo kwani wengi wao wanatumia leseni ambazo ni feki .

Aliongeza kuwa, dereva yoyote ambaye atabainika kutokuwa na cheti na akikutwa na leseni ni lazima aonyeshe na cheti kama hana ananyang’anywa leseni yake na kwenda kuleta cheti au kwenda shule ili kupata leseni iliyo sahihi.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka madereva hayo kufuata kanuni na sheria za barabara kwa kuvaa unifomu, kuwa na leseni na vyeti vyao ikiwa ni pamoja na kutosimamisha magari katika maeneo yasiyoruhusiwa ili kuweza kufuata sheria na kupunguza ajali mbalimbali za barabarani.

2 comments:

  1. watakagua vipi na wenyewe ndio wanaozitoa hizo feki? hawana lolote

    ReplyDelete
  2. Ni kweli Daraja C kwa sasa Tunauziwa laki sita baada ya kutoka VETA tuna kwenda wapi ? Hapa Dar kuna urasimu wa kutisha sana ni lazima tushwashike kununua kuliko kufuatikia Leseni kwa miezi 5 au 7

    ReplyDelete

Post Bottom Ad