Wanafunzi wa shule ya msingi Kising'a Isimani wilaya ya Iringa vijijini wakiwa wamebeba ndoo za maji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu jana majira ya saa 9.45 asubuhi muda ambao walipaswa kuwepo darasani kama walivyokutwa na mpiga picha wetu.
Na Blog ya Francis Godwin
TABIA ya uongozi wa shule ya msingi Kising'a Isimani wilaya ya Iringa kuwatumikisha kazi wanafunzi asubuhi wakati wa vipindi vya masomo imepingwa vikali na baadhi ya wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule hiyo na kuiomba wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kuingilia kati suala hilo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi leo kijijini hapo wazazi hao walisema kuwa uongozi wa shule hiyo ya msingi Kising'a kila siku kabla ya watoto kuingia madarasani wamekuwa wakiwatuma katika kazi mbali mbali ikiwemo ya kuchota maji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu.
Alisema Jonh Kalinga kuwa tayari wamepata kuulalamikia uongozi wa shule hiyo na kuukanya kacha kuwatumikisha watoto hao majira ya masomo ila bado vitendo hivyo vya wanafunzi kukatishwa vipindi na kwenda kufanya kazi za walimu vimekuwa vikiendelea.
Kwani alisema tayari wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi ilipata kupiga marufuku watoto kufanya kazi wakati wa vipindi vya masomo ila bado uongozi wa shule hiyo umeendelea kuwatumikisha watoto kazi .
Hivyo alitaka wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kufika katika shule hiyo ili kujua sababu ya walimu kuacha kuwafundisha watoto hao na badala yake kuwatumikisha katika kazi hizo.
Aidha wazazi hao walisema kuwa kila wakati wamekuwa wakichangia michango mbali mbali kwa ajili ya maendeleo ya shule hiyo ikiwemo michango ya ujenzi wa nyumba za walimu ila wanashangazwa kuona watoto wao hawasome na badala yake wanatumikishwa kufanya kazi ambazo zilipaswa kufanywa na wazazi.
Wanafunzi hao waliokutwa wakiwa wamebeba ndoo za maji walimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa katika shule hiyo kuna ujenzi wa nyumba ya mwalimu unaendelea na kuwa kila siku kabla ya kuingia madarasani wamekuwa wakitumwa kwenda kutafuta maji umbali wa nusu kilomita kutoka shuleni hapo ndipo waweze kuingia madarasani muda wa saa 4 asubuhi .
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta mkuu wa shule hiyo kwa ajili ya kujua sababu ya kuwatumikisha watoto hao kazi mbali mbali za mikono kabla ya kuingia madarasani ,mkuu huyo hakuweza kupatikana huku mwalimu mkuu msaidizi na mwalimu wa zamu katika shule hiyo wakiikimbia ofisi na kumwacha mwandishi wa habari hizi peke yake ofisini.
Kwa upande wake afisa elimu wa shule za msingi katika wilaya ya Iringa vijijini hakuweza kupatikana ili kulitolea ufafanuzi zaidi suala hilo baada ya kuwepo katika kikao.
No comments:
Post a Comment