ii ndiyo Medali ya Kumuenzi Sgt Gabriel Hugo Kisusange kama inayoonekana imetengenezwa kwa Crystal na si ya kuvaa bali ni ya kuwekwa nyumbani, Medali ya Dag Hammarskjold ilianzishwa na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, mwaka 1997 kwa Azimio namba 1121 (1997). Ni medali inayotolewa kwa wanajeshi, polisi au raia wa kimataifa ambao wamepotea maisha yao wakiwa katika shughuli za ulinzi wa Amani. Mwanadiplomasia na Kiongozi wa kwanza kupewa Medali hiyo alikuwa Ni Bw. Dag Hammarskjold ambapo familia yake ilikabidhiwa mwaka 1998. Dag Hammarskjold raia Sweden alikuwa Katibu Mkuu wa Pili wa Umoja wa Mataifa kati mwaka 1953 hadi 1961 alipopoteza maisha katika ajali ya ndege nchini Zambia akitokea nchini Congo ambapo alifanya mazungumzo ya kutafuta amani nchihi humo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki Moon, akimkabidhi Meja Wilbert Ibuge, Mwambata Jeshi katik Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa, Medali ya Dag Hammarskjold aliyotunukiwa Sgt Gabriel Hugo Kisusange ambaye alipoteza maisha wakati akihudumu katika Operesheni ya Ulinzi wa Amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudani. Ban Ki Moon alikabidhi medali hiyo kwa wanajeshi, polisi na raia 112 kutoka nchi 50 ambao wamepoteza maisha mwaka jana katika Operesheni mbalimbali za Ulinzi wa Amani. Utoaji wa Medali hizo ulikuwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka na kuwaenzi walinzi wa Amani, maadhimisho ambayo hufanyika kila Mei 29.
Meja Wilbert Ibuge akipeana mkono na Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani Bw. Herve Ladsous kati kati ni Katibu Mkuu Ban ki Moon, mara baada ya kukabidhiwa Medali ya Sgt Gabriel Hugo Kisusange aliyefariki mwaka jana akiwa katika Operesheni ya Ulinzi wa Amani huko Darfur. Sgt Gabriel Kisusange ni miongoni wa wanajeshi waliotunukiwa medali hiyo kuenzi mchango wao katika ulinzi wa amani.
Na Mwandishi Maalum
New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amewatunuku medali wanajeshi, polisi na raia kutoka nchi 50, ambao wamepoteza maisha mwaka jana,wakati wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi wa amani kupitia Operesheni za Kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.
Ban Ki Moon alitunuku medali hiyo ijulikanayo kama Medali ya Dag Hammrskjold siku ya Jumanne katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dag Hammarskjold hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Ikiwa ni kuadhimisha siku ya kimataifa ya walizi wa amani wa UM ambayo huadhimishwa Mei 29.
Kati ya watunukiwa hao ambao ni 112 wanawake na wanaume, yumo mwanajeshi kutola Jeshi la Wananchi la Tanzania ( JWTZ) Sajent Gabriel Hugo Kisusange aliyekuwa katika Jimbo la Darfur, nchini Sudan akihudumu katika jeshi la Mseto la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika maarufu kama UNAMID.
Medali ya Sgt Gabriel Hugo Kususange ilipokelewa na Meja Wilbert Ibuge Mwabata Jeshi katika Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa.
Medali ya Dag Hammarskjold ambayo imetengenezwa kwa Crystal na ambayo si ya kuvaa bali ya kuweka nyumbani ilianzishwa na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, mwaka 1992 kwa Azimio 1121 ( 1997)na inatolewa kwa wanajeshi, polisi au raia wa kimataifa ambao wamepoteza maisha wakihudumu katika ulinzi wa Amani
Akizungumza wakati wa hafla ya hiyo ,Ban Ki Moon amesema.“ Leo hii tunatoa heshima kwa mashujaa 112 ambao uhai wao ulikatishwa mwaka jana wakifanya kazi nchi ya Bendera ya Umoja wa Mataifa. Wanaweza kuwa wanajeshi, polisi au wafanyakazi wa kimataifa lakini hakuna tofauti miongoni mwao hasa ikizingatiwa mazingira magumu na ya hatari wanayokabiliana nayo wakati utekelezaji wa majukumu yao”.
Akaongeza kwamba, tofauti iliyopo kati ya shujaa na mtu wa kawaida, ni kwamba shujaa anajitolea na kukabiliana na hatari ili kuwaokoa wengine.
Akabainisha kwamba ni jambo jema na la muhimu kuwakumbuka na kuwapongeza walinzi wa amani wapatao 120,000 wanaohudumu katika misheni 17 duniani kote. Lakini ni wakati muhimu wa kuwakumbuka na kuwaenzi wale wote waliojitolea mhanga maisha yao kwaajili ya amani”.
“Wakati leo tukiwaenzi 112 waliofariki mwaka jana, wengine 31 wamekwisha kupoteza maisha yao mwaka huu” akasema Mkuu huyo wa UM.
“Lengo letu katika kulinda amani ni kulea utulivu wa kudumu katika maeneo yenye matatizo hadi pale ambapo kofia za Blue hazitahitajika tena. Tungependa kujitoa kwenye biashara hii” akasema Ban Ki Moon. Na kuongeza. “ Lakini mpaka itakapofika siku hiyo, sisi tutaendelea kuwa tayari kutoa msaada, na kuendeleza kazi ya wale tunaowakumbuka leo”.
Ban Ki Moon akatumia fursa hiyo kuzishukuru nchi zote ambazo zimejitolea wanajeshi wake, polisi na raia kushiriki katika Operesheni za kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.
Naye Mkuu wa Idara ya Operesheni ya Ulinzi wa Amani, Balozi Herve Ladsous yeye amesema jumla ya walinzi wa amani karibu 3000 wamekwisha kupoteza maisha tangu Umoja wa Amani ulipoanza jukumu hilo la kulinda amani mwaka 1948.
Akaongeza kuwa walinzi wa amani wanasaidia sana kuliwalinda mamilioni ya wananchi katika maeneo yenye vurugu na vita na kwamba jukumu hilo si kazi ndogo.
“ Tunakwenda kule ili kuwapa matumaini wananchi ambao wamepitia mateso makubwa ya vita na ambao wanatamani fursa ya kujenga upya maisha yao na kuishi kwa amani”.
Hata hivyo akasema kuwa inasikitisha sana pale inapotokea walinzi hao wa amani wanapokuwa walengwa na kushambuliwa wakati wanapotekeleza majukumu yao.
“ Hili halikubaliki ninatoa wito kwa kila mtu kuheshimu jukumu na mamlaka ya Helmeti ya Blue. Jukumu na mamlaka ya kuleta amani katika baadhi ya maeneo yenye matatizo duniani”. Akasisitiza
Ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu ni Ushirikiano wa Kimataifa katika Ulinzi wa Amani, ambapo kabla ya hafla ya utoaji wa Medali Katibu Mkuu Ban Ki Moon aliweka shada la Maua ikiwa ni ishara ya kuwaenzi mashujaa hao.

No comments:
Post a Comment