HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, February 11, 2012

Uchambuzi Wa Habari: Madaktari Waangusha Mbuyu

Ndugu zangu,

Ijumaa ya jana, tena asubuhi na mapema, nilisoma kichwa hicho cha habari kwenye gazeti la Mwananchi la mtandaoni . Kinavutia. Kinaacha tafsiri nyingi.

Habari hiyo ilitokana na mkutano Waziri Mkuu Mizengo Pinda na madaktari waliogoma. Mkutano ambao ulimalizika kwa kupatikana suluhu ya mgogoro, na hivyo basi, madaktari kumaliza mgomo wao.

Naam, ni heri hekima inayokuja kwa kuchelewa kuliko inayokosekana kabisa. Watanzania tunashukuru kwa Serikali na madaktari kutanguliza hekima na kufikia suluhu ya mgogoro.

Na hekima kubwa hapa ni kwa Serikali kutambua hekima za madaktari wetu kuwa hekima iliyohitajika ni kwa Serikali kuwasaidia madaktari katika kuuangusha mbuyu; Blandina Nyoni. Katika hilo tunawapongeza kwanza madaktari wetu kwa kuonyesha uzalendo mkubwa wa kuwa tayari kupambana hadi risasi ya mwisho na hatimaye kufanikiwa kuukata mbuyu ambao sasa ndio tunajua, kuwa ulikuwa mzizi wa mgogoro uliosababisha mgomo wa madakati na kuleta madhara makubwa.

Maana, ni heri kutibiwa na daktari aliyemaliza mgomo na kurudi kazini na moyo mkunjufu kuliko kutibiwa na daktari aliyelazimishwa kwa nguvu kurudi kazini huku akiwa bado na kinyongo.

Na Waziri Mkuu Pinda aliweka wazi sababu kuu tatu za Serikali kuwasimamisha kazi vigogo wawili wa Wizara ya afya Na Ustawi wa Jamii; Katibu Mkuu, Blandina Nyon na Mganga Mkuu wa Serikali, Dr. Mtasiwa.

Kwanza; ni kwa tuhuma za kuingiza nchini robo tatu ya vifaa bandia vya vipimo vya Ukimwi kutoka Korea Kusini.

Pili; tuhuma za kuanzisha kampuni ya kusambaza nguo kwa madaktari.

Tatu; kuiingiza kinyemela kampuni ya kufanya usafi ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbil.

Na Waziri Mkuu Pinda alisema mwenyewe, kuwa tuhuma hizo ni nzito zinazoidhalilisha Serikali na kamwe haitakuwa busara kuzifumbia macho huku Serikali ikiendelea kudhalilika. Pinda anasema;“Nimeamua kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu na Mganga Mkuu wa Serikali, ili kuweza kupisha uchunguzi,maana hizi tuhuma zinafedhehesha taifa."

Aliongeza; “Kwa upande wa Waziri na Naibu Waziri wa Afya, nimeshapeleka ushauri kwa Rais kutokana na yeye kuwa mwenye dhamana, siwezi kuliongelea hili hapa ila yule aliyewateua, atafanya maamuzi, najua kitakachofuata mnakijua,” alisema Pinda huku madaktari wakilipuka kwa shangwe na kuimba nyimbo ya mshikamano.(Mwananchi, Februari 10, 2012)

Na hapa nachukua fursa hii kumpongeza kwa ujasiri wake wa kuyatamka aliyoyatamka, na pia nampa Waziri Mkuu wangu Mizengo Pinda nyongeza ya sababu za wahusika kuchukuliwa hatua kali zaidi. 

- Wahusika wamesababisha madhara makubwa kwa jamii ikiwamo vifo vya wagonjwa vilivyotokana na mgomo ambao wao , kama wangewajibika ipasavyo, walikuwa na uwezo wa kuzuia usitokee.

-Wahusika wamewadhalilisha madaktari wetu na taaluma yao kwa ujumla.

- Wahusika kwa kuingiza nchini vifaa bandia ( feki) vya kupimia UKIMWI ni uhalifu mkubwa usiohitaji kuundiwa Tume bali kufunguliwa jarada la uchunguzi kwenye ofisi ya Upepelezi yenye kuhisika na uhalifu wa aina hiyo.

Matumaini yetu kwa siku chache zijazo?
Waziri mwenye dhamana na Naibu wake nao wakae pembeni maana tumewapa dhamana ya kuisimamia Wizara husika na wameshindwa kulisimamia hili la mgomo wa madaktari na hatimaye kutufikisha hapa tulipo. Wakikaa pembeni, kwa hiyari yao, au kwa kuombwa na Rais aliye na dhamana kuu, basi, watasaidia kurudisha imani yetu wananchi kwa Serikali. Watachangia pia kurudisha heshima ya Serikali na nchi.

Je, kwenye pori la mibuyu, yote imeangushwa?
Hapana, mibuyu iko mingi. Madaktari wetu wameangusha mbuyu mmoja tu. Na si kwa ’ shoka moja’. Mashoka yalikuwa mengi yakiwamo ya wanaharakati. Na jamii ikipiga sana kelele mibaya huanza kutingishika. Mibuyu haiangushwi bila kelele za wengi. Ni kama paka aliyeopoa kipande cha nyama chunguni. Ukimwandama sana atakitema. Na ikumbukwe, mibuyu porini inaanza kama mipapai.

Je, tunafanyaje basi kuitambua mibuyu inapokuwa katika hatua kama ya mipapai na hivyo tukaing’olea mbali?

Katiba, Katiba, Katiba…Ni kwenye Katiba Mpya inayokuja. Katiba iweke kipengelea kinachohakikisha , kuwa pale unapoonekana mbuyu, basi, kazi ya kuuangusha isihitaji mashoka mengi na hata kuchukua roho za watu. Inawezekana.

Maggid Mjengwa,
Iringa.
Februari 11, 2012
http://mjengwablog.com

1 comment:

Post Bottom Ad