HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 17, 2012

Rais Kikwete azindua madaraja makubwa mawili morogoro vijijini, aweka jiwe la msingi la soko, ahutubia katika mvua kubwa

Rais Jakaya Kikwete akielekea jukwaani kuhutubia wananchi huku mvua ikinyesha baada ya kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa soko la kijiji cha Mtamba, Morogoro na baadae kuzindua madaraja mawili makubwa katika mto Mtombozi, Matombo, na mto Magogoni katika barabara ya Kiganila-Mvuha na kukagua ujenzi wa barabara sehemu ya Kisaki, Msalabani.
Rais Jakaya Kikwete akiongea baada ya kuzindua daraja la mto Mtombozi tarafa ya Matombo wilaya ya Morogoro mjini leo.
Rais Jakaya Kikwete na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Joel Bendera wakimaliza kuvuka daraja jipya la Magogoni katika barabara ya Kiganila-Mvuha, Morogoro Vijijini mara baada ya Rais Kikwete kulizindua leo.
Rais Jakaya Kikwete na ujumbe wake na wenyeji wakipita juu ya daraja jipya la Mtombozi, Matombo, Morogoro vijijini alilolizindua leo.Picha na IKULU.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Januari 17, 2012 ametumia siku nzima akifungua miradi mbali mbali ya maendeleo Mkoani Morogoro katika siku ya pili ya ziara yake ya siku nne kukagua shughuli za maendeleo mkoani humo.

Rais Kikwete ameanza siku yake kwa kukagua ujenzi wa barabara ya lami ya kutoka Msalabani hadi kwenye njia panda ya Mto Mtombozi katika jimbo la uchaguzi la Morogoro Kusini, Wilaya ya Morogoro.

Aidha, Rais Kikwete amezindua daraja kwenye Mto Ruvu katika eneo la Magogoni. Daraja hilo la vyuma lina urefu wa mita 57.92 na limegharimu kiasi cha sh. Milioni 128.4, fedha zilizotolewa na Mfuko wa Maendeleo wa Serikali.

Ujenzi wa daraja hilo unatimiza ahadi ya Mheshimiwa Kikwete aliyoitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kufuatia kilio cha miaka mingi cha wananchi wanaioshi pande mbili za mto huo ambao walikuwa wanapata adha ya usafiri na kero ya kushindwa kuvusha mazao yao kuyafikisha kwenye masoko.

Rais Kikwete amezindua daraja jingine, zamu hii kwenye Mto wa Mtombozi, daraja ambalo linaunganisha vijiji saba vilivyo milimani katika Kata ya Mtombozi na vyenye wakazi wapatao 61, 115.

Jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo liliwekwa upya Juni 26, mwaka 2009, na Rais Kikwete mwenyewe baada ya ujenzi wake kusimama tokea mwaka 2002. Ujenzi wa daraja hilo umekwenda sambamba na ujenzi wa barabara ya kilomita 10.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 39 na lililogharimu sh 310,115,000, sehemu kubwa ikiwa ni fedha za Serikali litafuatiwa na miradi mingine kadhaa ya ujenzi wa madaraja na barabara katika eneo hilo, ili kupunguza shida ya usafiri na usafirishaji bidhaa na hasa mazao.

Rais Kikwete amemalizia siku yake ya leo kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko jipya katika Kijiji cha Mtamba, Tarafa ya Matombo ambalo ujenzi wake umekadiriwa kugharimu sh milioni 80.5 litakapokamilika.

Akizungumza na wananchi kwenye sherehe hiyo ya uwekezaji jiwe la msingi la ujenzi wa soko hilo, Rais Kikwete amesema kuwa kwa kuanza kwa ujenzi wa soko hilo, Serikali yake imetimiza ahadi zote ambazo alizitoa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Ahadi hizo zilikuwa ni pamoja na kupatia wananchi wa eneo hilo umeme, kuwapatia mtandao wa simu na kuwajengea soko kwa ajili ya kuuza mazao yao.

“Nafurahi kuwa sasa ahadi zetu zote kwenu kama zilivyotolewa wakati wa kampeni sasa zimekamilika. Tuliahidi umeme na sasa nguzo zimeanza kuwekwa, tuliahidi mtandao na sasa upo tuliahidi soko na sasa tunaanza kujenga soko. Yetu ni Serikali makini inayotimiza ahadi zake,” Rais Kikwete amewaambia wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad