HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, January 15, 2012

Mbunge awataka wapiga kura wake watambue kuwa uchaguzi umekwisha

Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini Bw. Stephen Ngonyani 'Almaarufu Profesa Majimarefu', akizungumza katika mkutano na wananchi wa kata ya Mazinde katika viwanja vya sokoni, ambapo aliwataka kutambua kwamba yeye kwa sasa ndiye mbunge kwa miaka mitano ijayo, wanatakiwa kuuunga mkono kuleta maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Bw. Erasto Sima (kulia) akizungumza katika mkutano wa mbunge wa Korogwe Vijijini Bw. Stephen Ngonyani 'Almaarufu Profesa Majimarefu' (kushoto) alipofika kwenye mkutano huo uliofanyika katika kata ya Mazinde ambapo mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi washiriki kazi za maendeleo katika kata yao.
Diwani wa kata ya Mazinde wilayani Korogwe Bw. Abdallah Mangare (Mwenye baraghashia kulia) akimwelewesha mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini Bw. Stephen Ngonyani 'Almaarufu Profesa Majimarefu' (aliyevaa nguo nyeusi), namna ambavyo sasa maji yanayotoka katika eneo hilo yanavyotakiwa kufikishwa katika makazi ya watu katika kijiji cha Mkumbara baada ya wananchi kuyatoa milimani.
katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Korogwe Vijijini Bi Lucie Mwiru, akizungumza katika mkutano wa mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini katika kata ya Mazinde alikokwenda kuwaeleza wananchi kwamba chama hicho kimekuwa kikitekeleza ilani yake iliyonadiwa mwaka 2010 hivyo wanatakiwa kushirikiana na viongozi kuleta maendeleo. Kulia kwa katibu ni Mwenyekiti wa CCM Korogwe Vijiji Bw. Nassor Malingumu.

Na Mashaka Mhando,Korogwe

WANANCHI wa kata ya Mazinde wilayani hapa, wametakiwa kutambua kwamba uchaguzi umekwisha na mbunge tayari amechaguliwa anawatumikia wananchi katika jimbo hilo hivyo wavunje kambi yao kwa lengo la kushirikiana naye ili aweze kusaidiana naye katika kuleta maendeleo katika kata hiyo.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara ulipofanyika kwenye uwanja wa sokoni, mbunge wa jimbo hilo, Bw. Stephen Ngonyani 'Almaruufu Profesa Majimarefu', alisema tangu amechaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, wananchi wa kata hiyo bado hawataki kumuunga mkono na badala yake kambi ya mgombea aliyemshinda anayetokea eneo hilo, bado inaendelea kufanya kazi na haitaki kumpa ushirikiano.

"Ndugu zangu uchaguzi umekwisha na mgombea wenu wa hapa, nimemshinda na mimi ndiye mbunge katika kipindi hiki cha miaka mitano, vunjeni kambi yenu, tushirikiane kuleta maendeleo sasa ya Mazinde, kung'ang'ana hakutawasaidia badala yake mtachelewesha maendeleo yenu," alisema Profesa Majimarefu aliyefuatana na Mwenyekiti wa CCM wa jimbo hilo Bw. Nassor Hemed 'Malingumu' pamoja na Katibu wa CCM Bi Lucie Mwiru.

Mbunge huyo alilazimika kufika katika eneo hilo, baada ya baadhi ya wananchi kulalamika kwamba mbunge huyo tangu amechaguliwa hajafika kwenye eneo hilo licha ya kupita barabarani kitendo ambacho mbunge huyo alikielezea kwamba kinatokana na taarifa anazopata kwamba wananchi hao bado wanamuunga mkono mgombea wao aliyetokea katika eneo hilo hivyo kuona kwamba hawataki kushirikiana naye.

Hata hivyo, baada ya mbunge huyo kuzungumza hivyo na wananchi kumtaka asahau suala hilo kwa kuwa sasa watamuunga mkono, mbunge huyo alisema atakutana na Mkurugenzi wa kampuni ya mkonge ya Mohamed Enterpresses Bw. Mohamed Dewji ili awapatie sehemu ya eneo katika shamba lake kwa ajili ya kujengwa kwa zahanati ya kata hiyo, soko na kituo cha mabasi hatua ambayo mbunge huyo kwa kushirikiana na Msajili wa Vyama vya siasa Bw. John Tendwa, tayari wameanza mchakato huo.

Pamoja na hali hiyo mbunge huyo alitembelea eneo ambalo wananchi wa kijiji cha mkumbara wamefikisha maji kutoka milimali na kumuomba mbunge huyo awasaidie kuyafikisha karibu na makazi ya watu kwa vile eneo ambalo maji hayo wanachota ni porini na ni hatari hasa kwa watoto wa kike ambapo mbunge huyo alikubali kuwasaidia kuyafikisha kwenye maeneo hayo.

Awali Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Bw. Malingumu aliwataka wananchi wa kata hiyo kujiandaa kuja kutoa maoni kwa tume itakayoundwa na Rais kwa ajili ya marekebisho ya katiba suala ambalo alisema linatakiwa wananchi hao kupitia katiba hiyo ili ukifika wakati huo waweze kueleza vifungu na vipengele ambavyo wanavitaka viongezwe au kupunguzwa.

Mkuu wa wilaya ya Korogwe Bw. Erasto Sima aliyefika baadaye kwenye mkutano huo wa mbunge, alifurahishwa na umati wa watu uliohudhuria mkutano huo na kwuataka kwamba wawe na utaratibu huo wa kwenda kusikiliza mikutano ya viongozi badala ya kusubiri nyumbani wakati mwingine maelezo yanayotolewa hupotoshwa, pia alitaka washiriki kazi za miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad