Na Mery Ayo,Arusha.
WANANCHI wa kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro mkoani Manyara
wameilalamikia serikali kuhusiana na hifadhi ya Taifa ya Tarangire
kuvamia ardhi ya kijiji hicho kwa lengo la kupanua hifadhi hiyo..
Ambapo hifadhi hiyo imekuwa ikivamia eneo hilo la kijiji bila kutoa
taarifa zozote kwa uongozi wa kijiji hicho hali ambayo imekuwa
ikiwaletea madhara makubwa kwa kukosa mahitaji yao muhimu huku mgogoro
huo bado unaendelea .
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa halmashauri ya kijiji hicho, Daniel
Melau wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua
hiyo ya hifadhi hiyo kuwaondoa wafugaji kwa nguvu kwenye ardhi yao
wakidai kuwa wanapanua hifadhi hiyo.
Aidha aliongeza kuwa hifadhi ya Taifa ya Ruaha imepanuliwa kutoka
kilometa za mraba 10,300 hadi kilometa za mraba 20,226 , ambapo
hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara nayo imepanuliwa kutoka kilometa za
mraba 330 hadi kilometa za mradi 648.7 ,ambapo katika upanuzi huu
vijiji vilivyo jirani na hifadhi vimekuwa vikipoteza ardhi na mali
nyingi.
Alisema kuwa, katika hatua hiyo TANAPA imekuwa ikihamisha mipaka
iliyowekwa kisheria huku ikichoma moto na kuteketeza nyumba za
wananchi wa kijiji hicho hali ambayo imekuwa ikileta mtafaruku mkubwa
katika jamii hiyo.
Alifafanua kuwa, mnamo tarehe novemba 18 mwaka huu , TANAPA iliwapiga
wanakijiji watano na kumlazimisha kijana aitwaye Isaya Nabana kula
gamba la nyoka .
'Tunafahamu kuwa Tanapa ina mpango unaojulikana kwa jina la ujirani
Mwema , ila tabia hii ya kuvamia mipaka kinyume cha sheria inakinzana
na maana nzima ya ujirani mwema ,ni jirani gani mwema anachoma moto
nyumba ya jirani mwenzake na kuhamisha mipaka pamoja na kuvuruga amani
katika jamii?'aliuliza Melau.
Hata hivyo Melau , alimtaka Rais Kikwete awafukuze kazi haraka Waziri
wa maliasili na utalii , Ezekiel Maige , pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa
TANAPA, Alan Kijazi kwa kuzidi kuzorotesha mahusiano kati ya serikali
ya Rais Kikwete na vijiji vinavyopakana na hifadhi za Taifa kama vile
kijiji cha Kimotorok.
Aidha aliitaka hifadhi hiyo, izuie wanyamapori wasikanyage katika
ardhi ya kijiji cha Kimotorok ,kwani mifugo ya wananchi inapoingia
hifadhini TANAPA hukamatwa , hali ambayo hifadhi hiyo imekuwa
ikijichukulia sheria mkononi huku ikifahamu fika kuwa muda mwingi kwa
mwaka maelfu ya wanyamapori wapo vijijini , ikiwa ni pamoja na kijiji
cha Kimotorok lakini wao wamekuwa hawawakamati .
Naye Mkurugenzi wa TANAPA Alan Kijazi akizungumza kwa njia ya simu
kuhusiana na swala hilo alisema kuwa, wao wanachofanya sio upanuzi wa
hifadhi bali ni uhakiki wa mipaka ambao inafanywa na Wizara ya Ardhi
na maendeleo ya makazi .
Alisema kuwa,TANAPA wao wanawawezesha tu katika kufanikisha zoezi hilo
ambalo linafanywa na wataalamu kutoka wizara husika ambao mwisho wa
siku watakuja na majibu sahihi kuhusiana na mipaka ilipo.
'Wanavyodai kuwa tumevamia eneo lao kwaupnuzi wa hifadhi sio kweli,
nafikiri hapa wananchi tu ndio hawajaelewa tunachofanya na wakumbuke
kuwa hifadhi sio mali ya TANAPA bali ni chombo cha serkali na sisi ni
wasimamizi tu'alisema Kijazi.
No comments:
Post a Comment