HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 21, 2011

Precision Air yaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam

Waziri wa Uchukuzi Mh. Omar Nundu akipiga kengele kama ishara ya kuorodheshwa rasmi kwa shirika la ndege la Precision Air katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE). Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi wa Precision Air Bw. Michael Shirima na mwakilishi wa mamlaka ya hisa nchini Tanzania Bw. Godfrey Malekano.

Precision Air PLC leo imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya hitimisho ya Uuzaji wa Hisa katika soko la Awali.

Uorodheshwaji huo uliendana na sherehe maalum uliohudhuriwa na mgeni rasmi Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Omar Nundu katika ukumbi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, pamoja na muasisi wa shirika hilo la ndege Bw. Michael Shirima, Mkurugenzi Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam Bw. Gabriel Kitua na mwakilishi wa Mamlaka ya Hisa Tanzania Bw. Godfrey Malekano.

Akizungumza wakati wa uorodheshwaji huo Waziri wa Uchukuzi Mh. Omar Nundu ameipongeza shirika la ndege la Precision Air kwa kuweza kuwa kinara wa usafiri wa anga nchini hadi kuweza kufikia hatua ya kuuza hisa zake pamoja na kujiorodhesha katika soko hilo la Dar es Salaam.

“Nawapongeza sana Precision Air, na napenda kuchukua fursa hii kutoa ahadi kama serikali kwamba tutajitahidi kuboresha sera na miundombinu yetu ili kuweza kuinua ushindani pamoja na kuwasaidia mashirika kama yenu kuweza kufanya biashara katika mazingira bora zaidi,” alisema Waziri Nundu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Precision Air Bw. Shirima alisema, “Kwanza kabisa, nawashukuru Mamlaka ya Hisa nchini Tanzania na Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa kutuongoza na kutulea kwa moyo wa dhati kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchakato huu. Tunaazimia kuendelea kushirikiana pamoja nanyi ili kuweza kutimiza lengo letu la pamoja la kuongeza thamani ya mwenye hisa katika kampuni; hasa hasa kwa wanahisa watarajiwa.”

Bw. Shirima pia aliwashukuru na kuwapongeza wanahisa wapya wa Precision Air; “Awali juu ya yote kuna wale washirika ambao pamoja na kwamba ni wawekezaji wapya, kuanzia leo katika tukio hili watakuwa wanahisa wa shirika hili la ndege. Napenda kusema ahsante na hongereni sana kwa ujasiri na sifa mlioweza kupatia shirika hili.”

Kwa upande wake naye Mkurugenzi Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam Bw. Gabriel Kitua alisema kwamba Precision Air ni shirika la 18 kuorodheshwa katika soko hilo, inayofanya Soko la Hisa la Dar es Salaam kushika nambari mbili kwa upande wa Afrika mashariki.

Jumla ya wawekezaji 7,056 (Elfu saba na hamsini na sita) walishiriki katika Uuzwaji wa Hisa katika Soko la la Awali (IPO) iliyoanza tarehe 7 Oktoba na kumalizika Novemba 4 2011.

Shirika limekusanya jumla ya shilingi za kitanzania bilioni 12 ambazo ni asilimia 43.18 ya kiasi kilichoombwa. Kwa kiasi kikubwa walioomba kununua hisa walikuwa wawekezaji wadogo wa ndani pamoja na Mashirika ya Kitanzania kama ilivyokusudiwa.

Shirika pia hapo nyuma liliwasilisha kwa Mamlaka husika mpango wa kifedha kuonyesha jinsi fedha zilizokusanywa zitakavyotumika na mikakati ya kujaza pengo kuhakikisha malengo ya shirika yanafanikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Pamoja na ukusanyaji fedha kuwezesha upanuzi, shirika pia lilikusudia kuongeza umiliki wa umma hasa wananchi wa Tanzania.

“Tunawashukuru wote walioshiriki kama ilivyothibitishwa na wingi wa ushiriki wao na tunafurahi kuwa zoezi la uuzaji wa hisa za shirika umefanikisha malengo yote mawili ya ukusanyaji wa mtaji na kuongeza wigo wa umiliki wa shirika kwa Watanzania,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Precision Air Bw. Alfonse Kioko.

“Ushiriki mkubwa wa Watanzania ni ushahidi wa kutosha kuwa wananchi wanaimani na matumaini kwa shirika lao la ndege. Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia kuwa uwekezaji wao utakuwa wa ufanisi,” Bw. Kioko aliongeza.

“Mpango wa kuongeza vituo vya usafiri na mtandao ulioko utaendelea. Pia shirika limeanzisha mpango kabambe wa kuimarisha huduma zake kwa wateja,” Kioko alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad