MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda (pichani), ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, ni miongoni mwa wajumbe walioteuliwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuunda kamati maalumu ya kukamilisha mchakato wa kupendekeza Vazi la Taifa.
Wengine wanaounda kamati hiyo itakayoanza kazi rasmi kesho ni Joseph Kusaga (Mwenyekiti), Angela Ngowi (Katibu) na wajumbe ni Habibu Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali, Makwaia Kuhenga na Ndesambuka Merinyo.
“Kamati itaanza kazi rasmi Desemba 15 mwaka huu na itatakiwa kukabidhi taarifa yake Februari 28 mwakani,” alisema Dk. Nchimbi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.
Alisema hatua inayofuata sasa ni kuwashirikisha wananchi kuhusu mapendekezo yaliyopo na hatimaye kupendekeza vazi mahususi litakalotambulisha utaifa wa Watanzania.
“Mchakato wa kupata vazi la taifa umeshapiga hatua kubwa, wabunifu wazalendo wa mitindo ya mavazi wameshashirikishwa na kutoa mapendekezo yao,” alisema na kuongeza:
“Utafiti wa namna mataifa mengine yalivyoweza kuteua mavazi yao ya kitaifa ulishafanyika na madhumuni ya kuwa na vazi la taifa ni kuongeza vitambulisho vya utaifa wa Watanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa utambulisho mwingine ni Ngao ya Taifa, Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, Lugha ya Taifa - Kiswahili, Mlima Kilimanjaro, Twiga na Mwenge wa Uhuru.
Alisema vazi hilo litakuwa rasmi kwa wanaume na wanawake na linatarajiwa kuongeza utambulisho zaidi kwa taifa kama ilivyo kwa mataifa mengine yakiwamo ya Swaziland, Ghana, Nigeria, Sudan, Ethiopia na Mali.
Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilianzisha mchakato wa kupata vazi la taifa mwaka 2004.
No comments:
Post a Comment