HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 29, 2011

Waziri Nchimbi kuwa mgeni rasmi kwenye fainali za pool taifa

Waziri wa Habari,Utamaduni,Michezo na Vijana 
Dr. Emmanuel Nchimbi
Na Mwandishi Wetu,Dodoma

WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Michezo na Vijana, Dr. Emmanuel Nchimbi kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha fainali za taifa za mashindano ya mchezo wa pool yanayojulikana kama 'Safari Lager National Pool Championship 2011'.

Fainali za mashindano hayo zinazoshirikisha mikoa 14 ya Tanzania Bara na kudhaminiwa na wadhamini wakuu wa mchezo wa pool nchini, kampuni ya bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, yanafanyikia kwenye ukumbi wa Kilimani Club mkoani hapa.

Mratibu wa mashindano hayo,Innocent Melleck amesema leo, mbali ya Waziri Nchimbi kuwa mgeni rasmi katika kilele cha fainali hizo pia kutakuwa na wageni mbalimbali wakiwemo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Melleck alisema kuwa tayari wametoa mwaliko kwa wabunge wote ambao wanatoka katika majimbo ya mikoa 14 inayoshiriki fainali hizo.

"Kila kitu kipo sawa hivyo wakazi wa Dodoma wafike kwa wingi katika kilele hicho kama ambavyo wamekuwa wakifanya tangu fainali hizo zilipoanza mapema wiki hii ili washuhudie timu itakayobeba ubingwa wa fainali hizo,"alisema Melleck.

Alisema kuwa kupitia udhamini wa bia ya Safari Lager fainali za mwaka huu zimeonekana kuwa na upinzani mkali tofauti na mwaka jana.

Melleck alisema kuwa hata timu ambazo hazikufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali zilionyesha ushindani mkubwa tofauti na misimu iliyopita.

Naye katibu mkuu wa chama cha mchezo huo nchini (TAPA), Amosi Kafwinga alisema kuwa kiufundi wachezaji wa timu zote mwaka huu wameonyesha ukomavu wa hali ya juu na hivyo kuleta changamoto zaidi katika mchezo huo.

Kafwinga aliongeza kwa kuwataka wakazi wa Dodoma kufika kwa wingi zaidi leo katika kilele cha fainali hizo ili kushuhudia viwango vya nguvu kutoka kwa wachezaji wa timu mbili zitakazocheza fainali.

Timu zilizofanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ni mabingwa watetezi mkoa maalum wa Kinondoni, Temeke, Ilala, Mwanza, Arusha, Morogoro, Mbeya na wenyeji Dodoma.

Wakati timu hizo zikifuzu kucheza robo fainali, timu sita ziliaga fainali hizo mapema ambazo ni Kagera, Shinyanga, Manyara, Iringa na Tanga.

Bingwa wa fainali hizo atajinyakulia fedha taslim Sh.milioni 5, mshindi wa pili Sh. Milioni 3.5, mshindi wa tatu milioni 2 na mshindi wa nne Sh.milioni 1.5.

Kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja wanaume bingwa ataondoka na Sh.500,000, mshindi wa pili Sh.250,000, mshindi wa tatu Sh.200,000, na mshindi wan ne Sh.150,000.

Na kwa upande wa wanawake bingwa atazawadiwa Sh.350,000, mshindi wa pili Sh.200,000, mshindi wa tatu Sh.150,000 na mshindi wan ne Sh.100,000.

Timu nane zilizoingia hatua ya robo fainali lakini hazikufanikiwa kuwa katika nafasi nne za kwanza kila moja itapewa Sh.500,000 na timu zote ambazo hazikuingia robo fainali kila moja itapewa Sh.250,000 ikiwa ni kifuta jasho cha kushiriki fainali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad