HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 8, 2011

Makamu wa Rais akiwa katika Kikao cha Maandalizi kwa ajili ya Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu masuala ya UKIMWI (UNAIDS)

Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wa pili kulia) akiwa katika Kikao cha Maandalizi kwa ajili ya Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu masuala ya UKIMWI (UNAIDS).  Wengine pichani ni Mhe. Juma Duni Haji (Mb), Waziri wa Afya -Zanzibar (wa pili kushoto), na Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (kushoto) na Mhe. Balozi Ombeni Sefue, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa (kulia).




Viongozi na wawakilishi mbalimbali kutoka Wizara ya Afya na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) wakimsikiliza Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kikao cha Maandalizi kwa ajili ya Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu masuala ya UKIMWI (UNAIDS).


NaTagie Daisy Mwakawago 
na  Glory Mziray

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu masuala ya UKIMWI wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UNAIDS).

Lengo la Mkutano huo ni kujadili changamoto zilizopo katika kupambana na UKIMWI, kutathmini hatua iliyofikiwa ya vita dhidi ya ugonjwa huo, na kupitia upya maazimio ya nchi wanachama ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2015.

Mkutano huo wa siku tatu umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia udhibiti wa UKIMWI na utafanyika jijini New York, Marekani kuanzia tarehe 8 hadi 10 juni mwaka huu katika Ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN-Headquarters).

Aidha ufunguzi wa Mkutano huo utahusisha hotuba mbalimbali za viongozi wakiwemo Rais wa Kikao cha 65 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Joseph Deiss, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-Moon na Mkurugenzi Mtendaji wa Programu ya Pamoja ya UKIMWI ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Bw. Michel Sedibe.
Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Bilal anatarajiwa kuelezea hali ya UKIMWI nchini Tanzania, mikakati iliyopo na athari za kiuchumi na kijamii nchini na duniani kote.

Wakuu hao wa nchi watajadili masuala ya kuimarisha huduma za afya, kinga, tiba, matunzo na misaada kwa wagonjwa, teknolojia na upatikanaji rahisi wa dawa. Aidha watajadili masuala ya ushirikiano wa dhati na wabia wa maendeleo, wito kwa nchi zinazoendelea kusimamia malengo ya nchi zao na kutoa rasilimali fedha zinazohitajika kupambana na UKIMWI.

Msisitizo utatolewa ili kuimarisha taarifa za elimu na mawasiliano, kupunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi UKIMWI na kusimamia afua za jinsia na UKIMWI.

Miongoni mwa viongozi walioambatana na Makamu wa Rais ni Waziri wa Afya – Zanzibar, Mhe. Juma Duni Haji (Mb), Waziri katika Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Mhe. Fatma Fereji (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb), Mbunge wa Viti Maalum- Iringa, Mhe. Ledianna M. Mng’ong’o (Mb) na viongozi wengineo kutoka Wizara ya Afya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad