Beatrice Mlyansi - Maelezo
TANZANIA itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Sita la Elimu Mtandao Barani Afrika litafanyika tarehe 25 hadi 27 Mei 2011 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Prof. Hamis Dihenga amesema, Kongamano hilo litashirikisha washiriki 2000 kutoka nchi 25 za Afrika na kwingineko duniani.
Kiongomano hilo litashirikisha Mawaziri wenye dhamana ya Elimu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Miundombinu, Utumishi wa Umma, Ajira na Maendeleo kutoka nchi 25 za Afrika.
Katibu Mkuu ameeleza kuwa, kongamano hilo litatoa nafasi kwa washiriki kujadili umuhimu wa elimu mtandao na kupanga mikakati ya kuboresha na kutumia elimu mtandao katika kuleta maendeleo kwa kutumia mbinu za kisasa za teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Amefafanua kuwa Kongamano hilo ni mahususi kwa ajili ya maendeleo, elimu na mafunzo kwa njia ya mtandao katika shule, vyuo na taasisi kwenye sekta mbalimbali lenye lengo la kuleta wataalamu katika Nyanja za maendeleo, elimu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia
“Mkutano huo utakuwa na faida mbalimbali kwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kupata ufahamu wa masuala ya matumizi ya elimu mtandao katika nyanja mbalimbali na kukuza mahusiano baina ya serikali ya Tanzania, taasisi za kimataifa na nchi nyingine pamoja na kukuza utalii.” Amesema Prof.Dihenga.
Makongamano ya aina hii yameshafanyika Addis Ababa Ethiopia mwaka 2006, Nairobi Kenya mwaka 2007,Accra Ghana 2008,Dakar Senegal 2009 na Lusaka Zambia mwaka 2010.

No comments:
Post a Comment