Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye akiwahotubia wakazi wa Manispaa ya Iringa katika uwanja wa Samora juzi wakati wa harambee ya kuchangia kituo cha watoto yatima (picha na Francis Godwin).
Na Francis Godwin ,Iringa
WAZIRI mkuu mstaafu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Frederick Sumaye ametaja baadhi ya mambo yanayoweza kuvuruga amani ya Tanzania iwapo hayatashughulikiwa huku akitaka mapamano ya kisiasa yafanyike kwa umakini mkubwa ili kuepusha vurugu.
Alisema kuwa amani ni rasilimali kubwa katika nchi yoyote na amani inaweza kutoweka na kuirudisha kwake ikawa ni kazi ngumu na kwa gharama kubwa iwapo misingi ya amani katika Taifa isipoheshimiwa na wananchi wote.
Sumaye aliyasema hayo jana wakati akichangia kiasi cha shilingi milioni 1 katika katika tamasha la nyimbo za Injili kwa ajili ya harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha Teknolojia ya habari na mawasiliano(ICT)kwa watoto yatima mkoa wa Iringa kupitia kituo cha Children Care Development Organization (CCDO) iliyofanyika kwenye uwanja wa Samora mjini Iringa.
Sumaye aliyataja baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuvuruga amani kuwa ni pamoja na ubaguzi wa aina mbali mbali, chokochoko za kiimani au dini ,mapambano ya kisiasa ,mtawanyiko wa mali au utajiri usiofaa na jambo jingine ni rushwa na ufisadi.
Hivyo aliitaka serikali kupambana kwa nguvu zote na vitendo vya Rushwa na ufisadi na kuwa penye rushwa mwenye haki hunyimwa haki yake stahiki na kupewa asiyestahiki kwa vile tu kutoa rushwa na kuwa rushwa na ufisadi vikiendelea kuota mizizi.
Akifafanua zaidi alisema kuwa chokochoko za kiimani au dini ni jambo la hatari sana katika nchi yetu na lazima likemewe na lidhibitiwe kwa nguvu zote kwani ubaguzi wa kidini ukiota mizizi amani huyeyuka kama barafu iliyoanikwa juani .
Kuhusu mapambana ya kisiasa Sumaye alitaka vyama kuendelea kupambana kisiasa huku vikilinda amani na utulivu na kuwa mapambano ya kisiasa yanahitaji utulivu na kuvumiliana kati ya vyama vinavyopingana ili visije vikaliingiza Taifa katika kupigana badala ya kupingana .
“…Nasema katika shughuli za kisiasa lazima taratibu za demokrasia zifuatwe …shughuli za siasa zifanyike kwa haki na uwazi na wanaoshindwa wakubali matokeo ya uchaguzi…pia suala la mtawanyiko wa mali au utajiri usiofaa…kama utajiri wan chi utaonekana umejikusanya kwa wachache na wengi wamebaki maskini hali ya amani itatoweka bila kujali kama walio nacho wamepata utajiri wao kihalali au lah …Hali hili kama ipo lazima irekebishwe na serikali ina taratibu za kufanya marekebisho kama hayo”
Sumaye alisema kuwa jambo jingine ambalo ni hatari kwa amani kwa Taifa ni vitendo ya rushwa na ufisadi ambavyo ni tatizo kubwa linaloweza kuvuruga amani ya Taifa iwapo haki itaendelea kutendeka kwa watoa rushwa na mafisadi pekee.
“Lazima rushwa na ufisadi upigwe vita kwa nguvu zote katika nyanja zote za kisiasa ,za huduma au za utoaji haki”.
Hata hivyo Sumaye alitaka watanzania kujenga moyo wa kuwasaidia yatima mbali mbali badala ya kuendelea kuongeza nguvu zaidi katika rushwa na vitendo vya ufisadi ambao ni hatari kwa amani ya Taifa.
Pamaoja na kumpongeza maratibu wa kituo hicho Majaliwa Mbongella kuwa na wazo nzuri hilo la kuwajali yatima bado aliwaomba watanzania kujitokeza kusaidia kituo hicho ambacho kinahitaji kiasi cha shilingi milioni 120 ili kuweza kutimiza ndoto yake ya kujenga kituo hicho cha habari na mawasiliano kwa yatima.
Awali mratibu wa kituo hicho Mbogella alisema kuwa kituo hicho kinataraji kuanza kwa kuwa na matawi mawili moja wilaya ya Makete na taji jingine mjini Iringa na kuwa kwa lengo ni kuwa na watoto 120 ambao wataanza kunufaika na mpango huo.
Hata hivyo alisema kuwa tayari kituo kilichosajiliwa kwa namba 000NGO/00003818/2009 kimepata ardhi zaidi ya ekari 25 katika eneo la Mkimbizi Iringa mjini 5 na Tanangozi Iringa vijijini 20 na kuwaomba watanzania wenye mapenzi mema watakaoguswa na maisha ya yatima kuingia katika blogu ya francisgodwin ama kuwasiliana na yeye (Majaliwa Mbogella)mratibu kwa namba 0752507519.
Mbogella alisema kuwa kituo hicho kitakuwa ni baba na mama wa yatima hao na kuwa mbali ya kuanza na yatima wa Makete na Iringa bado kituo kitasaidia watoto wa mikoa ya jirani kama Mbeya, Ruvuma ,Morogoro,na Dodoma ambako baadaye kutajengwa matawi pia.

No comments:
Post a Comment