HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 12, 2011

PENGO KATI YA WALIO NACHO NA WASIONACHO TISHIO KWA USALAMA WA DUNIA-TANZANIA

Mwakilishi wa Ubalozi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue akizungumza katika mkutano wa kamati maandalizi ya mkutano wa LDCs.


NA MWANDISHI MAALUM

NEW YORK-Ikiwa ni miaka kumi imepita tangu kupitishwa kwa mpango mkakati wa utekelezaji wa Brussels, uliolenga kuzikwamua nchi maskini kuliko zote duniani kutoka katika lindi la umaskini uliopindukia, hakuna hata nchi moja kati ya 48 iliyoweza kuhitimu na kuingia hatua ya pili.

Nchi hizo maarufu kama LDCs sasa zitakutana tena katika mkutano wake wa nne utakaofanyika jijini Instambul nchini Uturuki mwezi mei, kwa lengo la, pamoja na mambo mengine kufanya tathimini ya kwanini katika miaka hiyo kumi hakuna hata nchi moja iliyohitimu.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kamati maandalizi ya mkutano huo, uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ombeni Sefue, amesema mkutano huo ulenge katika kuibua mpango mkakati mpya wa utekelezaji wa Istambul wa kuongeza kasi ya kuzifanya nchi hizo maskini kuhitimu.

Akabainisha kuwa ingawa kila nchi imejitahidi kwa kiasi chake kutekeleza mpango mkakati wa Brussels lakini hali halisi inaonyesha kwamba hicho kilichofanyika hakitoshi na hivyo juhudi zaidi zinatakiwa.

Akaonya kwa kusema ni hali isiyokubalika kwamba, bado kuna kundi kubwa la watu ambao wanaishi katika hali ya umaskini wa kutupwa, huku idadi ya nchi maskini zaidi duniani haionyeshi kupungua kama ilivyotarajiwa. “ Lakini linalotisha zaidi ni kuendelea kuongezeka kwa pengo kati ya walionacho na wasionacho ndani ya nchi na kati ya mataifa na mataifa na hii inatishia usalama na utulivu si tu wa nchi moja moja lakini pia usalama wa kikanda na kidunia” anasema Sefue.

“ Lazima tuwe na lengo moja huko Instambul, nalo ni namna ya kuzisaidia LDCs ziweze kuhitimu na kuondokana na hali hii ya kusikitisha. Mchakato mzima wa mkutano huo na matokeo ya mkutano huo, kwa namna yoyote ile yasiingiliwe na mambo mengine isipokuwa nini cha kufanya kuzikwamua nchi hizo”. akasema Balozi Sefue.

Mwakilishi huyo wa Tanzania amewaeleza wajumbe wa mkutano huo wa maandalizi kwamba Tanzania inajua nini inataka katika mkutano huo.

“ Sisi Tanzania tunajua nini tunachokitaka kijiri huko Instabul. Tunataka fursa ya uhakika ya kujiletea maendeleo, na tunataka kuwaalika washirika wa kweli watakaotusaidia kuondoa vikwanzo vinavyozifanya nchi maskini zisihitimu na kuingia katika hatua nyingine ya maendeleo”.

Akisisitiza kile amabacho Tanzania inakitarajia kama matokeo ya mkutano huo, Balozi sefue anasema pamoja na mambo mengine, kwanza ni kutolewa kwa tamko la kurejea upya utashi wa kisiasa wa ushirikiano wa kuhitimu kama lengo la msingi kutoka nchi za LDCs, kutoka nchi zilizoendela, zinazoinukia kiuchumi na zile zinazoendelea.

Kwa mujibu wa Balozi Sefue, Tanzania ingepeda katika mkutano huo itolewa taarifa fupi inayotathimini utekelezaji wa mpango mkakati wa Brussels, ikielezea mafanikio, kuna lipi la kujifunza, na cha muhimu zaidi lipi linawezekana, lipi haliwezekani kwa nini na kwa vipi.

Aidha Balozi Sefue anasisitiza kuwa, Tanzania inataka kuona katika mpango mkakati wa utekelezaji utakaoibuliwa Instambuli unajielekeza katika kutoa mwelekeo wa kile ambacho nchi zenyewe maskini zinataka kifanyike ndani ya kila nchi na kikanda na kiwango cha ushirikiano na misaada kutoka wadau wa maendeleo ,ili kuharakisha mchakato huo wa kuhitimu kutoka kundi la nchi maskini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad