Na Mwandishi Wetu
MWANAFUNZI wa darasa la tatu shule ya msingi Mtongani Magadalena Pascali (13) amefariki dunia baada ya kugongwa na gari katika barabara ya Bagamoyo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Elias Kalinga alisema kuwa, tukio hilo lilitokea juzi majira ya nne asubuhi katika barabara hiyo eneo la Skanska wakati gari namba za usajili T 754 AIG aina ya Benzi Lorry, lililokuwa likiendeshwa na Slivester Komba (36) mkazi wa Tabata kumshinda na kumgonga mtoto huyo.
Aliendelea kusema kuwa, wakati gari hilo likitokea Mwenge kuelekea Tegeta, lilimshinda nguvu na kumgonga mtoto huyo aliyekuwa akitembea kwa miguu ambapo alifariki dunia papo hapo.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa Hospitali ya Mwanyamala na dereva aliyesababisha ajali anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi.
Katika tukio jingine, moto ulizuka ghafla katika kiwanda cha magodoro cha Vita Foam na kuunga baadhi ya mablock ya magodoro yaliyokuwa yametoka kwenye mitambo.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Mssime alisema tuki hilo lilitokea juzi majira ya saa kumi na mbili jioni wakati mablock makubwa yaliyokuwa yamesambazwa ili yapoe kufuatia kutolewa kwenye mashine ili baadae yakatwe yapatikane magodoro ndipo yaliposababisha moto huo.
Kamanda Mssime alisema kuwa chanzo cha moto huo inaaminika kutokana na joto kali la magodoro hayo ndipo yalipo lipuka na kuanza kuwaka moto huo.
Hata hivyo moto huo ulizimwa na kikosi cha zimamoto cha jiji kwa kushirikiana na kampuni ya binafsi ya Ultimate Security pamoja na wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment