MCHEZAJI wa zamani wa Yanga na timu ya taifa,Salvatory Edward ameeteuliwa kuwa kocha msaidizi wa kikosi cha Yanga.
Edward ambaye ni mchezaji wa zamani wa Sigara kabla ya kutua Yanga na kuichezea kwa mafanikio makubwa kabla ya kutundika daruga atasaidiana na Papic kuhakikisha Yanga inafanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Tanzania bara iliyopangwa kuanza rasmi Agusti 21 kwa timu hiyo kuanza ugenini kwa kucheza na Polisi Dodoma.
Akimtangaza rasmi jana, mwenyekiti mpya wa klabu hiyo Lloyd Nchunga alisema kamati yake imeamua kumteua nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa, ambaye pia alikuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa kilichotwaa ubingwa wa Chalenji mwaka 1994 kutokana na uwezo wake mkubwa wa ufahamu wa soka na atafanya kazi bega kwa bega katika masuala yote ya ufundishaji ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa Papic.
Mbali na Edward pia uongozi huo mpya umemteua Keneth Mkapa kuwa kocha mkuu wa Yanga B. Awali mkapa alikuwa meneja wa Yanga A.
Wakati huo huo uongozi huo mpya umelipa fadhila kwa kuwarejesha madarakani wagombea walioshindwa kwenye uchaguzi wao uliofanyika Julai 18 kwa kuwapa madaraka kwenye kamati mbali mbali walizounda.
Nchunga alisema kamati yake iliyoketi jana imewateuwa wajumbe watatu kuunda kamati ya utendaji ambao ni Seif Seif maarufu kama 'Seif Magari', Mbaraka Igangula na Pascal Kihanga.
Pia uongozi huo umemteua wakili Mark Antony kuwa mwenyekiti wa kamati ya nidhamu akisaidia na wakili mwenzake Rogers Ishengoma, wajumbe wakiwa ni mwamuzi Msafiri Mkeremi na Mbunge wa Dimani Zanzibar Hafidhi Alli.
Kamati ya Mipango mwenyekiti ni Charles Mgondo akisadiwa na Salum Rupia, David Mataka, Isaac Mazwile, Michael Malebo, na Abel Mtaro.
Kamati ya ufundi itasimamiwa na Mohamed Bhinda, atakayesaidiana na Ally Mayai 'Tembele', Sekilojo Chambua, Paul Malume, Edgar Chibura, Maneno Tamba na Abeid Abeid 'Falcon'
Kamati ya mashindano itaundwa na Seif Seif 'magari', Majid Seif, Abdallah Binkreb, Muzamili Katunzi, Albert Marwa, Moses Katabaro na Lameck Nyambaya wakati kamati ya kuratibu shuguli za matawi ni mpya na itaundwa na Tito Osoro, Kibwana Matokeo, Ali Kamtande, Theonest Rutashoborwa, Mzee Yusuf, Sarah Ramadhan na Athuman Fumo.
Nchunga ambaye kwa taaluma ni mwanasheria alisema kamati ya uchaguzi itabaki kama ilivyo ikiongozwa na Jaji John Mkwawa, makamu wake ni Ridhiwani Kikwete na wajumbe ni Philemon Ntahilaja, Yusuf Mzimba na Angetile Oseah.
No comments:
Post a Comment