HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 2, 2009

TRL Kunani??????

Wafanyakazi wa Kampuni ya Reli nchini (TRL) wakiandamana kwenda katika ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo kudai mishahara yao ya mwezi Novemba jana. Picha na Jackson Odoyo

Wafanyakazi TRL wamvamia mwekezaji

na Theopista Nsanzugwanko,Habari Leo

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), wamevamia na kuweka kambi katika Ofisi ya Menejimenti ya kampuni hiyo kumshinikiza mwekezaji, Kampuni ya Rites kuwalipa mshahara wa mwezi uliopita.

Hatua hiyo inafuatia mwekezaji huyo kushikilia msimamo wake kuwa hana fedha za kulipa mishahara labda baada ya siku nne au tano.

Jana saa tisa alasiri kulikuwa na ghasia kubwa wakati wafanyakazi hao walipoandamana na kuvamia ofisi hiyo na kutoa upepo kwenye magari matano ya viongozi wa menejimenti lakini waliishia nje bila kufika katika ofisi hizo baada ya kuzuiliwa na polisi wa Kituo cha Reli.

Polisi walitanda katika eneo la ofisi hizo za Menejimenti na kuhakikisha hakuna mfanyakazi yeyote anayefanikiwa kupandisha ghorofani kwenye ofisi za menejimenti.

Awali katika mkutano wao uliofanyika katika karakana za shirika hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Sylvester Rwegasira, aliwatangazia kuwa bado mwekezaji anashikilia msimamo wa kutokuwa na fedha za kuwalipa mishahara.

Baada ya kauli hiyo, wafanyakazi kwa kauli moja walikubaliana kwenda kwenye ofisi ya menejimenti zilizopo upande wa pili na kutoa upepo katika magari yenye namba za usajili T898 AZX, T760 AWG, T923 AVA, T180 AUN na T405 AVL.

Baada ya hatua hiyo, viongozi wa kampuni hiyo ambao ni wawekezaji walijifungia katika Ofisi ya Mkurugenzi na viongozi wa wafanyakazi wakiongozana na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Reli, Ruth Makelemo, waliingia katika kikao cha dharura.

Baada ya kikao hicho, Rwegasira aliwatangazia wafanyakazi waliokuwa nje ya Ofisi ya Mkurugenzi kuwa bado hakuna jitihada za kuridhisha kupata fedha hizo, hivyo wao viongozi watalala hapo ili kujadiliana huku wakiwasiliana na serikali kupata msaada.

“Tumejitahidi kuwasiliana na serikali na mpaka sasa wako kwenye kikao kuzungumzia suala hili hivyo ninawaomba tuonane kesho (leo) katika maeneo haya haya ya ofisi za menejimenti ili kufahamu jibu tutakalokuwa tumepata kwa muda uliobaki,” alisema Rwegasira.

Wafanyakazi hao waliokuwa wakimshangilia Katibu Mkuu wao walikubaliana na kuali hiyo ya kukutana asubuhi katika ofisi hizo ikiwa na maana kuwa hawataingia kazini leo.

Juzi, wafanyakazi hao waliitisha kikao cha dharura kujadili hatima ya mishahara yao ya Novemba baada ya uongozi wa wafanyakazi kupata barua kutoka kwa mwekezaji akidai hatalipa mishahara hiyo kutokana na kushuka kwa uzalishaji.

Lakini mbia mwenzake ambaye ni serikali inayomiliki asilimia 49 ya hisa amekwishatoa sehemu yake ya mishahara hiyo ambayo ni Sh milioni 522.

Kampuni hiyo imekuwa katika migogoro ya mara kwa mara tangu kuingia ubia kati ya serikali na Kampuni ya Rites ya India inayomiliki asilimia 51 ya hisa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad