Na Daniel Mjema,Moshi
MVUA kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana wilayani Same, imeleta maafa makubwa baada ya watu 30 kuhofiwa kufa kufuatia kitongoji chao kufukiwa na kifusi cha mlima uliopromoka na kuzifunika kabisa nyumba zao usiku wa manene wakiwa usingizini.
Kazi ya ukoaji ambayo ilikuwa ikifanywa kwa kutumia vifaa duni, yakiwemo majembe ilikuwa ikiendelea na hadi kufikia jana saa 11:00 jioni, miili ya watu 18 ilikuwa imeopolewa kutoka katika kifusi cha mlima huo ulioporomoka.
Akizungumza na Mwananchi kwa majonzi kwa simu kutoka Butiama, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anna Kilango Malecela alisema tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea saa 7:00 usiku wa kuamkia jana katika kitongoji cha Manja.
"Ni tukio baya ambalo halijawahi kutokea katika kitongoji hicho ni landslide (mlima ulioporomoka) imetokea usiku wakati wananchi wangu wamelala na kufunika kabisa nyumba saba ambazo hatujajua zilikuwa na watu wangapi" alisema Kilango.
Kilango alisema tukio hilo ambalo limetokea katika kitongoji hicho kilichopo kijiji cha Mamba Miamba limefanya jimbo hilo na wilaya nzima ya Same kuzizima kwa vilio na simanzi kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki na wananchi wa wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Kilango, wajumbe wote wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya ya Same wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Monica Mbega walikuwa katika eneo la maafa kusaidiana na wananchi katika shughuli ya uokoaji.
"Yaani ninachoweza kukuambia ni kuwa mlima ule umefunika nyumba zile zikawa (flati) huwezi kujua kama pale kulikuwa na nyumba. Ni tukio baya sana ambalo hatujawahi kulishuhudia" alisema Kilango kwa taabu na kwa simamzi.
Kilango pamoja na kutuma salamu za rambirambi kwa wananchi wake, jana alisitisha safari yake ya Butiama na kuanza kurejea jimboni kwake ili kuungana na wananchi kuomboleza msiba huo mkubwa kuwahi kulikumba jimbo humo.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Ibrahim Marwa alisema kuwa hadi kufikia saa 9:30 alasiri, idadi ya maiti waliokuwa wameopolewa ni 16 na kulikuwa na majeruhi nane waliookolewa katika jitihada zilizofanywa na wananchi waliofika mapema eneo la tukio.
"Kwa takwimu ambazo tumepata ni kwamba idadi ya waliokufa inaweza kufikia 25 hivi japo hatuna uhakika, lakini wapo majeruhi nane ambao wanahudumiwa hapa hapa na timu ya madaktari na wataalamu wa Afya kutoka Same" alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Alifafanua kuwa chanzo cha maafa hayo ni mvua nyingi zilizonyesha mfululizo kwa siku tatu na kuufanya mlima huo kushindwa kuhimili na kuporomoka na kuzifunika kabisa nyumba saba za wananchi wa kitongoji hicho usiku wa manane wakiwa wamelala.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mamba Miamba, Michael Chikira Mauya aliongea kutoka eneo la tukio kuwa inakadiriwa nyumba hizo zilizofunikwa zinakadiriwa kuwa na familia za watu kati ya 20 na 28.
"Mpaka sasa hivi (saa 6:00 mchana jana) tumefanikiwa kutoa miili 12 na tunakadiria katika nyumba saba zilizofunikwa kunaweza kuwa na watu hadi 28,Kwa kweli ni tukio ambalo ni baya sana hapa kijijini" alisema diwani Mauya.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Kata ya Mamba Miamba, Dia Mbwambo aliliambia Mwananchi kuwa katika maafa hayo amepoteza dada yake mkubwa aitwaye Rehema Kikera na mumewe Bakari Hoyange pamoja na watoto wao wanne.
Mbwambo alisema kutokana na namna miili ya marehemu ilivyoharibika, Mkuu wa Wilaya ya Same, Marwa aliyepo eneo la tukio, jana jioni aliwaruhusu ndugu jamaa na marafiki kuzika ndugu zao ili kuepusha miili hiyo kuendelea kuharibika zaidi.
Diwani huyo alisema ingawa wengi wa waliofariki anawafahamu, lakini asingependa kuwataja kwa majina bila ridhaa ya wanafamilia na kwamba, upo uwezekano wa kukosea majina na kuwachanganya na wale walio hai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng'hoboko, maofisa wengine wa polisi na askari wa vyeo vya chini na pia mkuu wa wilaya ya Same, Ibrahim Marwa walikuwa katika hekaheka za kuopoa miili ya waliokufa kutokana na janga hilo.
Tukio hilo limetokea wakati mvua ambayo imenyesha kwa siku tatu mfululizo katika kata za Maore, Ndungu, Kihurio, Bendera ikiwa imesababisha maafa makubwa na kusababisha vifo vya wanafunzi wawili ambao walisombwa na maji.
Kata nyingine zilizokubwa na mafuriko hayo ni Mtii, Bombo, Mpinji, Miamba ambazo ni kata za milimani, maeneo ambayo mvua hiyo imefanya uharibifu mkubwa zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Same, Juma Idd aliliambia Mwananchi kuwa wanafunzi hao wawili ambao hakuwataja majina yao, walikumbwa na maafa hayo wakati wakitoka shuleni Novemba 9, mwaka huu na ni wakazi wa Vijiji vya Ndungu na Mpinji.
Idd alifafanua kuwa mvua hizo zimeharibu miundombinu ya barabara hususan zile za maeneo ya milimani na kusababisha magari kupita kwa shida na mengine kukwama pamoja na mazao kama mahindi, ndizi na mpunga kuzolewa na maji.
Maafa hayo yametokea ikiwa ni miezi michache tangu Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kuonya kuanza kunyesha kwa mvua za El-Nino ambazo zinatabiriwa kuleta maafa makubwa hasa kwa wananchi wanaoishi mabondeni.
kwa habari zaidi bofya hapo

No comments:
Post a Comment