HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 15, 2009

KUELEKEA KATIKA KUSHEREHEKEA SIKUKUU YA EID,JESHI LA POLISI LATOA TAHADHARI KWA WANANCHI


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi nchini limewatahadharisha wananchi katika maeneo mbalimbali kujihadhari na vitendo vya hihalifu na wahalifu katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye siku kuu ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Tahadhari hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kamishna Msaidizi Abdallah Mssika (pichani), wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo.
Kamanda Mssika amesema kuwa uzoefu unmeonyesha kuwa mara nyingi wananchi wa dini zote wamekuwa wakisherehekea siku hii kwa shamra shamra mbalimbali ukiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi na wengine kuthubutu kuendesha magari kwa mwendo kasi na kupelekea ajali.

Amesema kuwa kutokana na uzoefu huo, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi mbalimbali wakiwemo walezi na wazazi, kutowaacha watoto wadogo pasipo na uwangalizi wa watu wazima ili kuepuka kugongwa na magari ama kuzama majini wakati kwenye fukwe za bahari na maziwa ama mabwawa.

Aidha wazazi na walezi wasiache nyumba zao bila uangalizi wa kutosha na pia kuepuka kuwaruhusu watoto wadogo kwenda kujazana kwenye kumbi za starehe kwa kuhofia kukosa hewa na kufariki dunia.

Kamanda Mssika amewatoa hofu wananchi na kusema kuwa watakuwa salama mwanzo hadi mwisho wa siku kuu hiyo na kwamba Jeshi hilo kwa kushirikiana na vikundi vya ulinzi wataimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya mijini na sehemu za kufanyia ibada na burudani na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu..

Amesema kuwa Jeshi hilo litatumia askari wake wa miguu, magari, Mbwa na Farasi katika kufanya doria kwenye maeneo korofi kwa lengo la kuwahakikishia wananchi usalama wao pamoja na mali.

Hata hivyo Jeshi la Polisi linawakumbusha wafanyabiashara kuepuka kusafirisha fedha nyingi kwa wakati mmoja kutoka eneo moja hadi lingine lakini ikiwa ni lazima kufanya hivyo wanashauriwa kutoa taarifa kwa wakuu wa Polisi ili kupatiwa askari wa kuwasindikiza ili fedha zao ziwe salama.

Kwa upande wa Walinzi wa majengo ya viwanda, ofisi na maghala ya kuhifadhia mali na bidhaa mbalimbali zikiwemo za madukani wametakiwa kujiepusha na vishawishi vya kufadhiliwa vyakula na vinywaji kutoka kwa watu wasiowafahamu wawapo kwenye malindo yao ili kuepuka kupewa simu ama madawa ya kulevya na kuibiwa.

Amewataka pia Madereva wa magari ya abiria na madereva wa Taxi kujiepushe na mambo ya ulevi na kwenda mwendo wa kasi ambao unaweza kusababisha ajali za barabarani. Pia abiria wa magari hayo a wanatakiwa kutoa taarifa kwa askari wa usalama barabarani ili waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili kwa kukiuka mashariti ya udereva.

Aidha amewakumbusha pia wamiliki na madereva wa magari madogo waepuke kutoa lifti kwa watu wasiowafahamu ili kuepuka kuporwa magari na kusababisha hasara kwa wamiliki wake.
Amesema kuwa pamoja na uchache wa skari wa Jeshi hili hapa nchini, Jeshi hilo limejipanga kuwashirikisha wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kuimarisha doria na kufanya kwa pamoja katika kuwahakikishia wananchi usalama wao.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwezi huu, Kamanda Mssika, amesema kuwa hivi karibuni, Polisi waliweza kuokoa mali zote zilizokuwa zimeporwa kwa abiria Mkoani Dodoma baada ya kulisimamisha gari walilokuwa wakisafiria majambazi wakiwa pamoja na mali walizowapora abiri wa mabasi na magari mengine madogo.

Amesema kuwa mara baada ya askari hao walisimamisha gari hilo, majambazi hayo kila mmoja alikurupuka kwa lengo la kutoroka lakini wakakutana na kundi kubwa la watu waliokuwa wakiwasaidia Polisi katika msako na hatimaye kuwapiga hadi kuwaua papo hapo majambazi sita na Polisi walifanikiwa kuipata silaha iliyotumika katika tukio hilo.

Huko mkoani Kigoma kamanda Mssika amesema kuwa Polisi waliokuwa wakifuatilia wizi wa vifaa vya ujenzi wa barabara na juzi walifanikiwa kuwakamata watu watatu kwa tuhuma za kuiba kiasihicho kikubwa cha vifaa vya mradi wa kampuni ya ujenzi ya CHICCO inayojenga barabara mkoani humo.

Amewataja watuhumiwa waliokamatwa wakiwa na mali hizo majumbani kwao ni Edwin Michael (24) na Hamiisi yasini(32) wakazi wa Kazegunga na Siri Jastine(27), mkazi wa Burera.
Mali iliyookolewa ambayo thamani yake bado haijajulikana imetajwa kuwa ni matairi sita ya magari makubwa, mapipa mawili ya mafuta ya dizeli, mifuko mitatu ya simenti na chokaa mifuko miwili, nindo 50 za milimita 16 kila moja na fedha taslimu shingi 1,110,000 fedha ambazo zinahisiwa zimepatikana kutokana na mauzo ya baadhi ya vifaa vilivyoibwa.

Mkoani Kagera Polisi walipambana kijasiri na majambazi waliotaka kuteka magari katika pori la Kimisi mkoani humo, na kuwaua majambazi wawili na kuwajeruhi wengine wanne kabla ya kukimbia katika tukio hilo polisi tumefanikiwa kupata bunduki tatu aina ya SMG, mabomu mawili ya kutupwa kwa mkono pamoja na makasha matano ya risasi yaliyosheheni jumla ya risasi 133 za SMG ambazo pia zinatumika katika silaha za SAR.

Amesema mafanikio haya yanatokana na utayari wa askari kutokana na mtego ulioandaliwa vema na Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Kagera Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Peter Richard Matagi.

Amesema Majambazi hayo yaliuawa wakati yakiwa katika harakati za kuteka magari ya abiria kwa lengo la kuwapora mali zao na mara walipotakiwa kujisalimisha kwa Polisi yalikaidi na kuanza kuwafyatulia askari risasi kabla ya Polisi kujibu na kuwaua majambazi hayo mawili na kuyajeruhi mengine manne na kutupa silaha walizokuwa nazo.

Wakati wa mkutano huo, Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Mererani mkoani Manyara Mrakibu wa Polisi Bw. Lazaro Mambosasa na kachero Koplo fadhili Juma wa ambaye ni Afisa Polisi Kata ya Chikongola. Walielezea uzoefu wao waliopelekea kufanikiwa katika kuunda vikundi vya ulinzi na kupunguza yhalifu katika himaya zao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad