
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameielekeza Wizara ya Kilimo kushughulikia kwa haraka kero za wakulima, zikiwemo malipo ya madeni ya mauzo ya Tumbaku, mgawanyo wa shamba la uzalishaji wa mbegu -Namtumbo, upatikanaji wa pembejeo na bei ya Mahindi, ili kuwawezesha wakulima kuanza uzalishaji kwa wakati na kuongeza tija.
Ameelekeza hayo wakati wa ziara yake Wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma tarehe 11 Novemba 2026, ambapo amesisitiza utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutenga sehemu ya shamba la uzalishaji wa mbegu kwa wananchi wa eneo husika na kuagiza hatua hiyo itekelezwe mara moja.
Shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 6,618.43 linajumuisha hekta 1,366.03 zinatumika kwa makazi ya wananchi;, hekta 3,580.39 zinatumiwa na Wakala ya Mbegu za Kilimo (ASA) kwa kuzalisha mbegu, na hekta 1,672.01 zimeelekezwa kutengwa kwa wananchi kufanya shughuli za kilimo.
Kuhusu madeni ya wakulima wa Tumbaku, Makamu wa Rais ameelekeza Kampuni ya 3H kukamilisha malipo ya deni la Dola za Marekani 450,000 ifikapo mwisho wa Novemba 2026. Kwa mujibu wa kampuni hiyo, vyama 38 kati ya 43 tayari vimeshalipwa, huku vyama vitano vilivyobaki vikiwa vimepokea asilimia 50 ya madai yao.
Akizungumzia suala la mahindi, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amesema Serikali imeongeza bei ya ununuzi kutoka Shilingi 450 hadi 500 kwa kilo na kwamba Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) uko tayari kuanza mara moja ununuzi wa mahindi katika Ghala la Namtumbo baada ya kukamilisha maandalizi yote muhimu.Kuhusu mbolea, Waziri Chongolo amewataka mawakala wa mbolea za ruzuku Namtumb kuzingatia bei elekezi ya Serikali ya Shilingi 93,000 hadi 95,000 kwa mfuko.
Ziara hiyo imewahamasisha wakulima kuendelea kuingia mashambani na kuongeza uzalishaji, huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto zilizobaki ili kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa Taifa.

.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment