Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umeingia kwenye ushirikiano wa kimkakati na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa lengo la kutumia nguvu ya vyombo vya habari vya kidijitali kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu kuhusu hifadhi ya jamii, pensheni na uwekezaji.
Ushirikiano huo umejadiliwa wakati timu ya maofisa wa PSSSF ilipotembelea Makao Makuu ya TBN, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, ambapo pande hizo zilikubaliana kushirikiana katika utoaji wa taarifa sahihi na uelimishaji wa umma kupitia majukwaa ya kidijitali.
Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo wenye zaidi ya wanachama 200 nchini na Diaspora una uwezo mkubwa wa kuifikisha elimu hiyo kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ya wanachama wake.
Msimbe alisema TBN iko tayari kutumia uzoefu na wigo wake kuwasaidia wananchi kuelewa huduma zinazotolewa na PSSSF, huku akisisitiza umuhimu wa wanachama wa mtandao huo kupata mafunzo ya kina kuhusu hifadhi ya jamii ili waweze kutoa taarifa sahihi na zenye tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za mfuko kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi kwa kushirikiana na wadau wa habari.
Njaidi alisema PSSSF itafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa na TBN, akisisitiza dhamira ya mfuko kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana kuhusu pensheni, hifadhi ya jamii na uwekezaji unaofanywa kwa manufaa ya wanachama na Taifa.
Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo una uzoefu mkubwa katika habari za kidijitali na uko tayari kuwa kiungo kati ya PSSSF na wananchi.
“TBN ipo tayari kushirikiana na PSSSF kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha nyepesi, sahihi na inayoeleweka kupitia majukwaa ya kidijitali,” alisema Michuzi.
Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kuwajumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo, huku TBN ikiwasilishwa na Beda Msimbe, Rahel Pallangyo, Cathbert Kajuna na Issa Michuzi.








No comments:
Post a Comment