Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP-Centre), David Kafulila, amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kupitia uwekezaji wenye tija na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kafulila amesema ushirikiano huo unapaswa kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza ajira na kuchochea ujenzi wa uchumi shindani na endelevu, kwa kuhusisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo, Septemba 25, 2026, mkoani Pwani, wakati wa Kongamano la Fursa za Uwekezaji na Ushiriki wa Sekta Binafsi katika Miradi ya Ubia (PPP), lililolenga kukuza uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Richard Kayombo, amesema kongamano hilo litasaidia kuwaelimisha wafanyabiashara na wananchi kuhusu fursa za uwekezaji, huku likichochea ajira na maendeleo ya Mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TNCC, Oscar Kissanga, amesema makongamano ya uwekezaji yanapaswa kuzaa matokeo yanayoonekana, ikiwemo kufungua fursa mpya za uwekezaji, kuwaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji, pamoja na kuongeza tija katika sekta binafsi na uchumi wa Taifa.



No comments:
Post a Comment