HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 24, 2026

MKUYU AFRICA YAWATAKA DIASPORA KUMILIKI NYUMBA NCHINI

 Kampuni ya Mkuyu Africa imewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi kutumia sehemu ya kipato wanachopata kupitia ajira na biashara kuwekeza nchini, hususan katika kumiliki ardhi, nyumba na majengo ya biashara kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.


Kauli hiyo imetolewa wakati wa uzinduzi wa mpango maalumu wa Miliki Ardhi Diaspora, uliozinduliwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Vifaa vya Ujenzi (BUILDEXPO) 2026, jijini Dar es Salaam.

Mpango huo unalenga kuwawezesha Watanzania wanaoishi ughaibuni kushiriki katika fursa za umiliki wa mali nchini, huku wakiwa bado wanafanya kazi na kutafuta kipato nje ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, alisema mpango huo umeandaliwa kwa lengo la kuwasaidia Watanzania wa diaspora kuanza kujenga msingi wa maisha yao ya baadaye mapema.


“Kwa sasa una nguvu ya kutafuta, lakini baada ya miaka kadhaa utatamani kurudi nyumbani Tanzania. Ndiyo maana tunataka kuwasaidia kuanza kumiliki mali mapema,” alisema Othman.

Alisema Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanaweza kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini kuwekeza katika mali isiyohamishika kulingana na uwezo wao na mipango yao ya kifedha.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, aliwataka wawekezaji nchini kuongeza uwekezaji katika uanzishaji wa viwanda, hususan viwanda vinavyozalisha vifaa vya ujenzi.

Alisema uwekezaji huo ni muhimu katika kuongeza uwezo wa Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Dkt. Akwilapo pia aliwataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi kutumia fursa zilizopo kuwekeza nchini na kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mazingira ya uwekezaji nchini yanaendelea kutoa fursa katika sekta mbalimbali, ikiwemo uzalishaji wa vifaa vya ujenzi ambavyo ni muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kupitia mpango wa Miliki Ardhi Diaspora, Mtanzania anayeishi nje ya nchi anaweza kuanza mchakato wa kumiliki nyumba, ardhi au mali nyingine nchini akiwa bado ughaibuni. Baadhi ya miradi pia ina utaratibu wa malipo kwa awamu kulingana na masharti yaliyowekwa.

Akizungumza katika maonyesho hayo, Salim Abubakar alisema hapo awali baadhi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi walikumbana na changamoto baada ya kuwatuma ndugu zao fedha kwa ajili ya kujenga nyumba, kununua viwanja au kuanzisha biashara.

Alisema baadhi yao waliporejea nchini baada ya muda walikuta mipango ya uwekezaji waliyoiacha mikononi mwa ndugu zao haijatekelezwa, hali iliyosababisha migogoro na kutokuaminiana ndani ya familia.

“Watu wengi waliokuwa nje ya nchi walikuwa wakiwatumia ndugu zao fedha kwa ajili ya kujenga nyumba, kununua viwanja au kuwekeza katika biashara. Lakini baadhi yao waliporudi walikuta hakuna nyumba, hakuna kiwanja wala uwekezaji waliokusudia, jambo lililosababisha watu kugombana ndani ya familia,” alisema.

Abubakar alisema uwepo wa mipango inayowawezesha Watanzania wa diaspora kufuatilia na kusimamia uwekezaji wao nchini unaweza kuwasaidia kupanga na kusimamia umiliki wa mali kwa utaratibu unaoeleweka.

Mkuyu Africa imeeleza kuwa mpango wa Miliki Ardhi Diaspora unalenga kujenga daraja kati ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi na fursa za umiliki wa mali nchini, huku ukiwahimiza kuanza maandalizi ya maisha yao ya baadaye mapema badala ya kusubiri hadi watakaporejea Tanzania.

Hata hivyo, wataalamu wa uwekezaji wanashauri wanunuzi kufanya uhakiki wa nyaraka za umiliki, mikataba, eneo la mradi, masharti ya malipo pamoja na gharama nyingine kabla ya kufanya uamuzi wa kununua mali.


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, mara baada ya uzinduzi wa mpango wa Miliki Ardhi Diaspora wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Vifaa vya Ujenzi (BUILDEXPO) 2026 yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad