Na Mwandishi Wetu, Tanga
WANAFUNZI wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) wamebuni mifumo ya kidijitali inayolenga kurahisisha usimamizi wa taka na matumizi ya maji kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano.
Mwanafunzi wa Fani ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Fatuma Ismail, amebuni mfumo unaowezesha vifaa vya kuhifadhi taka kutoa taarifa kwenye simu janja pindi taka zinapofikia kiwango cha kujaa, hivyo kurahisisha hatua za kuziondoa.
Akizungumza katika Banda la MNMA kwenye Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga.
Fatuma amesema mfumo huo unalenga kusaidia katika utunzaji wa mazingira na kudumisha usafi.
Amesema mfumo huo unaweza kutumiwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo majumbani, kwa kufungwa kwenye vifaa vya kuhifadhi taka ili kutoa taarifa kwa njia ya simu janja pindi taka zinapokuwa zimejaa.
Fatuma amesema mfumo huo pia unaweza kusaidia Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kufuatilia hali ya maeneo ya kuhifadhi taka na kupata taarifa kwa wakati ili kuchukua hatua stahiki.
Amesema matumizi sahihi ya mfumo huo yanaweza kupunguza msongamano wa taka katika maeneo mbalimbali kutokana na kuwepo kwa mawasiliano ya moja kwa moja kati ya kifaa cha kuhifadhi taka na mtumiaji.
Kwa upande mwingine, mbunifu wa MNMA, Godfrey Kasembe, amebuni kifaa kinachoweza kufungwa kwenye mita za maji na kutoa taarifa za matumizi ya maji moja kwa moja kwenye simu janja au kompyuta bila mhusika kwenda kusoma mita hizo.
Kasembe amesema MNMA imekuwa ikimsimamia kwa karibu katika hatua zote za ubunifu huo, kuanzia wazo hadi kufikia hatua ya kutengeneza kifaa.
Amesema mfumo huo utasaidia mamlaka za maji kupunguza gharama na muda unaotumika kwa watumishi kwenda nyumba kwa nyumba kusoma mita, kwa kuwa taarifa za matumizi zitapatikana moja kwa moja kupitia mfumo huo.
Ameongeza kuwa teknolojia hiyo pia itasaidia kupunguza uwezekano wa udanganyifu katika usomaji wa mita kwa kuwa taarifa za matumizi zitakuwa zikiwasilishwa moja kwa moja kwenye mfumo. Kasembe amesema kwa sasa mfumo huo upo katika hatua za usajili ili kukamilisha taratibu na kuanza kutumika.



No comments:
Post a Comment