Na Mwandishi Wetu
WADAU wa teknolojia na usimamizi wa intaneti wametakiwa kutumia fursa zinazotokana na mtandao huo kwa maendeleo ya jamii badala ya kuutumia kwa matusi, chuki, udhalilishaji na vitendo vinavyoweza kuathiri maslahi na haki za watu wengine.
Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa Tanzania Internet Governance Forum (TIGF), Dkt. Nazarius Kirama, wakati wa Mkutano wa 13 wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti Tanzania, unaojadili masuala mbalimbali yanayohusu matumizi, usalama na mustakabali wa intaneti nchini.
Kirama amesema mkutano huo umewakutanisha wadau kutoka serikalini, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, wataalamu na wasomi kutoka vyuo vikuu kwa lengo la kujadili namna ya kukuza matumizi salama na yenye tija ya intaneti, huku masuala ya akili mnemba (AI), ujumuishi wa kidijitali, ulinzi wa taarifa binafsi na intaneti yenye kasi yakiwa miongoni mwa mada zinazojadiliwa.
Amesema Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti Tanzania lilianza mwaka 2005 na ni sehemu ya mfumo wa mijadala ya usimamizi wa intaneti unaofanyika katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa, uliolenga kutoa nafasi kwa wadau kujadili namna bora ya kusimamia mustakabali wa teknolojia hiyo.
Kirama amesema licha ya intaneti kuwa nyenzo muhimu ya kufikisha huduma, taarifa na fursa kwa watu wengi, baadhi ya watumiaji wamekuwa wakiitumia vibaya kwa kutoa lugha za matusi, chuki na vitendo vinavyoweza kuharibu maslahi ya wengine, akisema tabia hizo zinaakisi changamoto zilizopo katika jamii.
“Jamii iliyopo kwenye mitandao ya kijamii haikutoka mbinguni, inatokana na jamii yetu. Kwa hiyo yale mambo yanayofanyika mtaani yanaweza pia kufanyika mtandaoni,” amesema Kirama, huku akiwataka watumiaji kujenga utamaduni wa kujidhibiti badala ya kutegemea udhibiti wa mamlaka pekee.
Amesema wananchi wanapaswa kutafakari thamani wanayoipata kutokana na matumizi ya intaneti na kuhakikisha fedha wanazolipia huduma hiyo zinatumika kwa shughuli zenye manufaa, ikiwamo kujenga jamii, kuelimisha, kuongeza fursa za kiuchumi na kuunganisha watu. “Intaneti ya bure bila faida ni kujiletea umaskini.
Kwa nini utumie fedha kulipia intaneti halafu uitumie kumtukana mtu? Intaneti yenyewe ina gharama,” amesema.
Katika mkutano huo, Mwanaharakati wa masuala ya teknolojia na miundombinu ya TEHAMA, Damilola Kihinde, amewataka wazazi, hospitali na wahusika wengine wanaokusanya au kuhifadhi taarifa za watoto kuhakikisha taarifa hizo zinalindwa ili kuepusha matumizi mabaya, udhalilishaji na uvunjwaji wa haki zao za msingi.
Kihinde amesema mtoto mdogo hawezi kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya taarifa zake, hivyo mzazi akiwa mlezi na mlinzi wake wa kwanza ana wajibu wa kuhakikisha picha na taarifa zake hazishirikishwi au kutumiwa kwa namna inayoweza kumletea madhara.
Amesema pia hospitali, ambazo zinaweza kuwa wadhibiti wa taarifa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, zinapaswa kuweka mifumo imara ya kulinda taarifa za watoto na wagonjwa.
Amesisitiza kuwa ulinzi wa taarifa binafsi za watoto ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa wazazi, hospitali na wahusika wengine, huku maslahi bora ya mtoto na haki yake ya faragha yakipewa kipaumbele.
Kwa upande wake, Pious Sylvester, Mratibu wa Ushirikiano wa Shirika la African Child Project, amesema jamii inapaswa kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa za watoto, hasa katika kipindi ambacho matumizi ya mitandao ya kijamii yanaendelea kuongezeka.
Amesema Tanzania pia inapaswa kuendelea kushiriki katika majukwaa ya kikanda na kimataifa kuhusu usimamizi wa intaneti ili kupata fursa ya kujadili changamoto na kutoa mchango katika mijadala ya mustakabali wa teknolojia.

.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment